Usafirishaji nje bidhaa za Iran waongezeka kwa asilimia 68
Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Biashara ya Iran amesema kuwa, usafirishaji nje bidhaa za Iran umeongerzka kwa asilimia 68 katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu wa 1400 wa Hijria Shamsia ikilinganishwa na wakati kama huu katika mwaka uliopita wa Kiirani.
Shirika la habari la IRIB limenukuu Bw. Hamid Zadboom akisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu wa Kiirani wa Hijria Shamsia, Tehran imeuza nje tani milioni 30 za bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 10 na milioni 700. Kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 68 ikilinganishwa na muda kama huo mwaka jana yaani 1399 Hijria Shamsia.
Amesema, maeneo makuu ambayo zimeuzwa bidhaa za Iran katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ni China, Iraq, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Uturuki na Afghanistan ambapo bidhaa zilizoingia Iran katika kipindi hicho, nyingi zake zimetokea Imarati, China, Uturuki, Ujerumani na Uswisi kwa utaratibu.
Siku chache zilizopita pia, Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, licha ya kuweko vikwazo vikali vya Marekani dhidi ya Iran, lakini Tehran inaendelea kuzalisha na kuuza nje mafuta yake.
Bijan Namdar Zangeneh alisema hayo katika kikao cha 181 cha OPEC na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Iran iko chini ya vikwazo na mashinikizo makubwa mno ya Marekani na licha ya kwamba vikwazo hivyo vimeisababishia matatizo sekta ya mafuta, lakini uzalishaji na usafirishaji nje mafuta unaendelea.
Vile vile alisema, siasa za Iran zimejikita kwenye kuimarisha ushirikiano na misimamo ya pamoja ya nchi wanachama wa OPEC na kuweko ushirikiano baina ya wazalishaji na watumiaji wa nishati ya mafuta.