Taarifa ya Kikao cha Mazungumzo Baina ya Waafghani mjini Tehran
Mazungumzo ya amani ya Afghanistan ambayo yamekuwa yakifanyika baina ya Waafghani hapa Tehran kwa siku mbili yamemalizika kwa kutolewa taarifa ya pamoja.
Kwa mujibu wa taarifa pande mbili zilizoshiriki katika mazungumzo hayo ya amani ambayo yalianza Jumatano zimemaliza mkutano na kutoa taarifa yenye vipengee sita.
Taarifa hiyo imesema pande mbili zilizoshiriki katika mazungumzo hayo awali kabisa zimeishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nia yake njema katika jitihada zake za kusaka amani Afghanistan na kuandaa kikao hicho.
Aidha taarifa hiyo imesema pande zote mbili zinadiriki kuwa iwapo vita vitaendelea, Afghanistan itapata madhara na kwa msingi huo vita si suluhisho na kwamba pande zote zinapaswa kujitahidi ili kufanikisha suluhisho la kisiasa na la amani kwa mgogoro wa nchi hiyo.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, mazungumzo ya Tehran yamefanyika katika mazingira ya kirafiki na masuala yote muhimu yamejadiliwa kwa kirefu na uwazi.
Hali kadhalka taarifa hiyo imesema kikao hicho cha Tehran kimekuwa fursa mpya ya kuimarisha mchakato wa utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Afghanistan.
Mazungumzo hayo baina ya Waafghani yamewashirikisha wawakilishi wa serikali ya Afghanistan na pia wawakilishi wa ngazi za juu wa kisiasa wa kundi la Taliban na yamefanyika Tehran chini ya uwenyeji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Iran iko tayari kusaidia mchakato wa amazungumzo baina ya mirengo ya Afghanistan kwa lengo la kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Katika hotuba yake leo wakati wa kumalizika mazungumzo hayo, Zarif ametoa wito wa kusitishwa vita Afghanistan.