Makamu wa Rais: Iran ndio nchi inayoongoza kisayansi na kiteknolojia katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i72148-makamu_wa_rais_iran_ndio_nchi_inayoongoza_kisayansi_na_kiteknolojia_katika_eneo
Makamu wa Rais anayehusika na masuala ya sayansi na teknolojia amesema, ijapokuwa Iran ilijiwekea malengo ya kuwa dola linaloongoza katika sekta za sayansi na teknolojia ifikapo mwaka 1404 hijria shamsia, lakini hivi sasa tayari imeshalifikia lengo hilo muhimu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 08, 2021 23:11 UTC
  • Makamu wa Rais: Iran ndio nchi inayoongoza kisayansi na kiteknolojia katika eneo

Makamu wa Rais anayehusika na masuala ya sayansi na teknolojia amesema, ijapokuwa Iran ilijiwekea malengo ya kuwa dola linaloongoza katika sekta za sayansi na teknolojia ifikapo mwaka 1404 hijria shamsia, lakini hivi sasa tayari imeshalifikia lengo hilo muhimu.

Sorena Sattari ameeleza hayo Alkhamisi akiwa katika ziara ya kukagua bustani ya sayansi na teknolojia ya mkoa wa Alborz na akaongeza kuwa, katika nyuga maalumu za utaalamu kama wa nano, selishina na anga za mbali, Iran imepiga hatua kubwa sana kiasi kwamba idadi ya mashirika yanayoshughulika na sekta hizo imeshapindukia elfu sita. 

Sattari amesema, mashirika ya Iran ya elimu za utaalamu (knowledge-based) yanaendelea kustawi na kuongezeka kwa kasi ya kuridhisha na akabainisha kuwa, harakati ya upigaji hatua katika uga wa uchumi unaotegemea elimu za utaalamu imeshaanza nchini.

Baadhi ya vifaa vilivyoundwa nchini kwa kutumia teknolojia ya nano

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya sayansi na teknolojia ameeleza pia kwamba, katika masuala kama ya virusi vya corona, kuanzia siku za awali vilipozuka virusi hivyo, zilichukuliwa hatua nzuri katika mashirika ya elimu za utaalamu kuhusiana na vifaatiba pamoja na vifaa vya upimaji.

Sattari ameashiria pia ustawi na ongezeko la mashirika ya elimu za utaalamu nchini Iran kutoka elfu sita hadi nane na akaongeza kuwa, mengi kati ya mashirika hayo yamekomaa kiuwezo na kufikia hatua ya kuwa mashirika ya kuaminika yenye uwezo wa kutangaza bidhaa zao kwenye masoko.../