Iran yavunja mtandao wa magaidi wa MOSSAD
Vikosi vya Wizara ya Intelijensia ya Iran vimefanikiwa kusambaratisha mtandao wa magaidi wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad) magharibi mwa nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha kupambana na ujasusi cha wizara hiyo amesema vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu vimewatia nguvuni magaidi hao waliojipenyeza nchini kupitia mpaka wa magharibi.
Ameeleza bayana kuwa, mbali na kukamatwa maajenti hao wa MOSSAD, lakini maafisa usalama nchini wamefanikiwa pia kunasa idadi kubwa ya silaha na mada za miripuko zilizoingizwa nchini kimagendo na magaidi hao wenye mfungamano na Wazayuni.
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Wizara ya Intelijensia ya Iran amesema majasusi hao wa MOSSAD ya Israel wametiwa mbaroni kutokana na kuwa macho vyombo vya usalama vya taifa hili.
Amesema baadhi ya silaha zilizonaswa katika operesheni hiyo ni pamoja na bunduki za aina kadhaa ikiwemo ya AK-47, maguruneti, mada za miripuko na risasi.
Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha kupambana na ujasusi cha Wizara ya Intelijensia ya Iran amesema magaidi hao walikuwa wamekula njama ya kutumia silaha hizo kutekeleza mashambulizi ya kigaidi na pia kuzipenyeza katika maandamano yanayoshuhudiwa katika mkoa wa Khuzestan.
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Khuzestan, kusini magharibi mwa Iran wamekuwa wakifanya maandamano kwa siku kadhaa kulalamikia uhaba wa maji. Tayari Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameviagiza vyombo husika kuhakikisha vinashughulikia kwa uzito mkubwa matatizo ya wakazi wa mkoa huo wa kusini magharibi mwa Iran.