Balozi wa Uingereza Tehran aiomba radhi serikali na wananchi wa Iran
Balozi wa Uingereza mjini Tehran ametoa maelezo kuhusu picha iliyosambazwa mitandaoni akiwa pamoja na balozi wa Russia na akaiomba radhi serikali na wananchi wa Iran.
Simon Shercliff, balozi wa Uingereza mjini Tehran, jana Alkhamisi alifika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ambapo mbali na kueleza alivyosikitishwa na suutafahamu iliyojitokeza, amesema, "mbali na ninavyoiheshimu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wananchi wake wanaoheshimika na historia ya nchi hii, ninasisitiza kuwa, hakukuwa na nia na madhumuni yoyote mabaya nyuma ya kadhia hii."
Balozi wa Uingereza mjini Tehran ameongeza kwamba, kilichokusudiwa na mabalozi ni kukumbushia tu umoja wa Urusi na Uingereza dhidi ya Ujerumani ya Manazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Shercliff aidha amesema, ana matumaini kwamba katika kipindi cha utekelezaji wa majukumu yake hapa Tehran, ataweza kusaidia katika kustawisha uhusiano wa nchi mbili kwa msingi wa kuimarisha kiwango cha kuaminiana na kuheshimiana baina ya pande mbili.
Kufuatia kusambazwa picha ya mkutano uliofanywa hivi karibuni kati ya mabalozi wa Russia na Uingereza hapa mjini Tehran, Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha Ulaya Magharibi katika wizara ya mambo ya nje ya Iran, jana alimtaka balozi wa Uingereza afike wizarani hapo, ambapo mbali na kumfahamisha kwamba, hatua hiyo iliyotonesha hisia na ghera ya utaifa ya wananchi wa Iran haikubaliki, alisistiza pia kwamba, katika zama zote za historia watu wanaoheshimika wa Iran wamethibitisha kila mara kuwa wanapinga vikali harakati yoyote inayotokana na fikra na hisia za kiistikbari na kusimama imara dhidi yake.
Balozi wa Russia mjini Tehran, Levan Dzhagaryan naye pia jana hiyo hiyo aliitwa wizara ya mambo ya nje ya Iran na kutakiwa atoe maelezo kuhusiana na picha hiyo.
Katika mazungumzo na Alireza Haqiqiyan, naibu waziri na Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha Eurasia, Dzhagaryan alisema, kusambazwa picha hiyo kulifanywa kwa madhumuni ya kukumbushia umoja tu baina ya Urusi na Uingereza dhidi ya jeshi la Kinazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na wala haina makusudio mengine yoyote dhidi ya Iran.
Katika picha yao hiyo ya pamoja, mabalozi wa Russia na Uingereza wanaonekana wamekaa mahali palepale ambapo Rais Franklin Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill na Kiongozi wa shirikisho la kisovieti la Urusi Joseph Stalin walikaa na kupiga picha ya ukumbusho baada ya "Mkutano wa Tehran" ambao waliufanya mwaka 1943 ndani ya ubalozi wa Urusi hapa mjini Tehran bila ya kutoa taarifa yoyote kwa serikali ya Iran wakati huo.
Viongozi waandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Mohammad Javad Zarif na Spika wa Bunge Mohammad Baqir Qalibaf waliwataka mabalozi wa Russia na Uingereza waombe radhi kwa kitendo hicho.../