Iran: Ugaidi ni matokeo ya uingiliaji wa kijeshi na njama za kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i73920-iran_ugaidi_ni_matokeo_ya_uingiliaji_wa_kijeshi_na_njama_za_kisiasa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ni muhanga mkubwa wa aina zote za ugaidi tangu kuasisiwa kwake na kwa msingi huo, inawaunga mkono manusura wote wa vitendo vya kigaidi.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 25, 2021 08:30 UTC
  • Iran: Ugaidi ni matokeo ya uingiliaji wa kijeshi na njama za kisiasa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ni muhanga mkubwa wa aina zote za ugaidi tangu kuasisiwa kwake na kwa msingi huo, inawaunga mkono manusura wote wa vitendo vya kigaidi.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo katika hotuba yake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka na Kuwaenzi Wahanga wa Ugaidi na kuongeza kuwa, ugaidi na misimamo ya kufurutu ada ni matokeo ya upikaji majungu na njama za kisiasa za baadhi ya nchi.

Amesema machungu ya familia za wahanga wa ugaidi hayapaswi kubebwa tu na jamaa za wahanga wa vitendo hivyo, bali jamii ya kimataifa inapaswa kuhusika.

Khatibzadeh amesema, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelengwa kwa kila aina ya ugaidi ukiwemo ugaidi wa kisiasa, kiuchumi, na wa ummati, na kwa hiyo inasimama na wahanga wa ugaidi ikiwa na uzoefu wote huo wenye thamani."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema dunia haipaswi kupuuza nafasi ya mabeberu katika kukuza na kushajiisha 'biashara ya vita' duniani na hususan katika eneo la Asia Magharibi. Amesema: Leo hii jamii za Wamagharibi zinafahamu kuwa uingiliaji wa kijeshi wa Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi katika eneo umefungua mlango wa kuongezeka makundi ya kigaidi kama ISIS na Jabhatu Nusra katika eneo.

Askari wa US nchini Iraq

Ameeleza bayana kuwa, mbali na kuuawa kigaidi wanasayansi wa Kiirani, lakini pia jeshi la kigaidi la Marekani lilimuua shahidi aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Luteni Jenerali Qassem Suleimani.

Kuhusu kuondoka vikosi vya Marekani nchini Afghanistan, Khatibzadeh amesema, "hawa wanasiasa hawakubali kubeba dhima wakati moto wa vita unapowaka, lakini wanaondoka na kukimbia, bali hata wanadanganya bila aibu kuhusu mafanikio waliyoyapata."