Iran yalaani mashambulio ya Kabul, ISIS yatangaza kuhusika nayo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali mashambulio ya kigaidi yaliyotokea nje ya uwanja wa ndege wa Kabul nchini Afghanistan jana Alkhamisi.
Saeed Khatibzadeh ametoa salamu za rambirambi za serikali na watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa taifa la Afghanistan na kuwaombea rehma na maghufira ya Mwenyezi Mungu walioaga dunia katika hujuma hiyo ya kigaidi, sanjari na kuwatakia shifaa ya haraka majeruhi wa mashambulizi hayo.
Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesikitishwa sana na kuuliwa bila ya hatia raia wa kawaida katika mashambulio hayo ya Kabul, wakiwemo wanawake, watoto na vijana.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa: Tunatumai serikali jumuisha itaundwa huko Kabul haraka iwezekanavyo, ili mamlaka husika zichukue jukumu la kulinda maisha na mali za Waafghani.
Wakati huohuo, kundi la kigaidi la ISIS limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ambayo ni ya kwanza kutokea mjini Kabul tangu rais Ashraf Ghani aitoroke nchi; na mji mkuu huo wa Afghanistan kudhibitiwa na kundi la Taliban mnamo tarehe 15 Agosti.
Kupitia shirika lake la habari za kipropaganda la Amaq, genge hilo la kigaidi na kitakfiri limetangaza kuhusika na miripuko hiyo ya jana.
Taarifa ya ISIS iliyotumwa kwenye ukurasa wake wa Telegram imesema: Mwanachama wa Daesh aliyekuwa amejifunga mabomu alifanikiwa kupenya na kuufikia ummati mkubwa wa wakalimani na washiriki wa jeshi la Marekani katika kambi ya Baran karibu na Uwanja wa Ndege wa Kabul na kujiripua.
Kabla ya ISIS kutoa tamko hilo, maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon walisema, wanaitakidi kuwa kundi la kigaidi la ISIS ya Khorasan ndilo lililohusika na miripuko hiyo ya jana iliyotokea katika mazingira ya mtafaruku na msongamano wa watu waliomiminika katika uwanja wa ndege wa Kabul kwa lengo la kuihama nchi.
Wakati huohuo, Rais Joe Biden amesema kamwe Marekani haitosahau wala kusamehe mashambulio hayo, na kwamba italipiza kisasi.