Qalibaf: Kuondoka kwa madhila Afghanistan, dalili ya kusambaratika US
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74328-qalibaf_kuondoka_kwa_madhila_afghanistan_dalili_ya_kusambaratika_us
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema hatua ya Marekani kuondoka kwa fedheha na madhila nchini Afghanistan imeonesha wazi kuwa Washington iko katika mkondo wa kusambaratika na kupoteza nguvu na ushawishi wake katika uga wa kimataifa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 06, 2021 03:04 UTC
  • Qalibaf: Kuondoka kwa madhila Afghanistan, dalili ya kusambaratika US

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema hatua ya Marekani kuondoka kwa fedheha na madhila nchini Afghanistan imeonesha wazi kuwa Washington iko katika mkondo wa kusambaratika na kupoteza nguvu na ushawishi wake katika uga wa kimataifa.

Muhammad Baqir Qalibaf alisema hayo jana Jumapili katika hotuba yake Bungeni na kusisitiza kuwa, miaka 20 ya Marekani kuikalia kwa mabavu Afghanistan imeonesha kuwa, Washington si tu imeshindwa kuifanya nchi hiyo ipige hatua katika uga wa uchumi na miundombinu, lakini pia imepelekea nchi hiyo kushindwa kupata jambo la msingi kwa jamii yoyote ile, ambalo ni usalama.

Qalibaf ameeleza kuwa, "Wananchi wa Iran wanawaunga mkono watu wa jamii zote Afghanistan na makabila yao, na irada ya Jamhuri ya Kiislamu ni irada ya Waafghani."

Spika wa Bunge la Iran amebainisha kuwa, Afghanistan ina mustakabali wenye kung'aa, na Wairani wataendelea kusimama na Waafghani mkabala wa madola ya kibeberu yanayojaribu kuibua ukosefu wa usalama na uthabiti nchini humo.

Wanajeshi wa US wakiondoka kwa fedheha Afghanistan

Marekani imeshaondoa rasmi askari wake wote nchini Afghanistan baada ya miaka 20 ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo na kuisababisha maafa na hasara kubwa. Ndege ya mwisho ya Jeshi la Marekani aina ya C-17 iliondoka Uwanja wa Ndege wa  Kimataifa wa Kabul Jumatatu iliyopita. 

Marekani na waitifaki wake walianza mchakato wa kuondoa askari na watumishi wao wapatao 123,000 kutoka Afganistan kuanzia mwezi Julai mwaka huu.