Iran: Kutumiwa kisiasa IAEA kutatufanya tutoe jibu tofauti
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74340-iran_kutumiwa_kisiasa_iaea_kutatufanya_tutoe_jibu_tofauti
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya vikali Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya kufanya mahesabu ghalati katika mkutano wake ujao na kusisitiza kuwa, kutumiwa kama jukwaa la kisiasa taasisi hiyo kutailazimisha Tehran itoe jibu tofauti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 06, 2021 02:51 UTC
  • Iran: Kutumiwa kisiasa IAEA kutatufanya tutoe jibu tofauti

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya vikali Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya kufanya mahesabu ghalati katika mkutano wake ujao na kusisitiza kuwa, kutumiwa kama jukwaa la kisiasa taasisi hiyo kutailazimisha Tehran itoe jibu tofauti.

Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo leo Jumatatu katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari na kueleza kuwa,  pande husika za makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hazipaswi kuchukua hatua na kufuata mkondo ambao utaathiri mazungumzo ya Vienna ya kujaribu kuyahuisha mapatano hayo ya kimataifa.

Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita wa Agosti, IAEA katika ripoti yake mpya ilidai kuwa Iran imeongeza kasi ya urutubishaji madini ya urani.

Kuhusu uwezekano wa kuja hapa nchini hivi karibuni Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Khatibzadeh amesema, "masuala ya kiufundi kati ya IAEA na Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran yataelezwa na msemaji wa AEOI."

Khatibzadeh amebainisha kuwa, mazungumzo ya mara kwa mara baina ya Iran na IAEA yanaendelea; na kusisitiza kuwa shughuli zote zote za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinaenda sambamba na mkataba unaopiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia NPT na chini ya usimamizi wa taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia pia kuhusu mazungumzo ya Vienna ya kujaribu kuhuisha JCPOA na kukariri kuwa, mazungumzo hayo yanapaswa kukidhidi mahitaji na matakwa ya Iran, kwa mujibu wa vipengee vya JCPOA na Azimio Nabari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kabla ya hapo pia, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alionya kuwa, Washington inapaswa itambue kuwa haina chaguo jengine isipokuwa kuacha uraibu wake wa vikwazo na kutumia lugha na mwenendo wa heshima katika kuamiliana na Tehran.