"Kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu ni hatua ya kistratajia"
Rais wa Iran amesema wazo la kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu lililobuniwa na Imam Khomeini (MA), Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni hatua ya kistratajia katika ulimwengu wa Kiislamu.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 35 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran leo Jumanne, Rais Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa, suala la umoja linaweza kuwasilishwa kwa serikali za Kiislamu kwa kuepuka migawanyiko na taarifa zinazoweza kuibua mifarakano baina ya Waislamu.
Sayyid Raisi ameeleza kuwa, mfumo unaotawala dunia hautaki kuona umma wa Kiislamu ukiungana, na hivi sasa, baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wanautazama Uislamu kama kizingiti cha kufikia malengo yao.
Huku akiwakumbuka na kuwaenzi Meja Jenerali Qassem Soleimani na Ayatullah Mohammad Ali Taskhiri kutokana na jitihada zao za kisiasa na kielemu za kuondoa mifarakano na kuukurubisha pamoja umma wa Kiislamu, Rais Raisi amesema madola ya kibeberu yamebuni, kuyafadhili na kuyapa silaha makundi ya kitakfiri kwa lengo la kuuparaganyisha umoja wa Waislamu duniani.

Ameeleza kuwa, mbali na kutumia makundi ya kigaidi na kitakfiri kuwagawa Waislamu katika misingi ya madhehebu, lakini ulimwengu wa Magharibi unatumia mbinu ya kupanda mbegu za chuki miongoni mwa Waislamu, na vile vile kusimika serikali dhaifu zitakazopigania maslahi ya Wamagharibi katika nchi za Waislamu, badala ya maslahi ya umma wa Kiislamu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Wamagharibi wameshindwa kufikia malengo yao, jambo ambalo limemfanya kijana wa Kiislamu ambaye huko nyuma alitamani kulia na kuishi katika mazingira ya Kimagharibi, hii leo anataka kuwa huru na kujikomboa.
Mkutano wa 35 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza leo hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja, chini ya kaulimbiu ya "Umoja wa Kiislamu; Amani na Kuepukana na Mifarakano."