Maendeleo ya Iran katika teknolojia ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76644-maendeleo_ya_iran_katika_teknolojia_ya_nyuklia
Akiba ya madini ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 imezidi kilo 210 na ile iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60 hapa nchini imefikia kilo 25.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2021 08:43 UTC
  • Maendeleo ya Iran katika teknolojia ya nyuklia

Akiba ya madini ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 imezidi kilo 210 na ile iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60 hapa nchini imefikia kilo 25.

Hayo yalisemwa Ijumaa iliyopita mjini Tehran na Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la  Iran (AEOI), Behrouz Kamalvandi katika maonyesho ya mafanikio ya Iran katika uga wa nyuklia.  

Mafanikio makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika  teknolojia ya nyuklia ni katika fremu ya utumiaji wa nishati hiyo kwa malengo ya amani. Iran inaamini kuwa, silaha za nyuklia ya silaha zote za maangamizi ya umati zinapaswa kuharibiwa kikamilifu kote duniani. Ripoti za kuaminika zinasema kuwa, kuwepo kwa makombora na silaha zaidi ya elfu 14 za nyuklia ni hatari kubwa kwa wanadamu na sayari ya dunia. Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA), Bertrand Goldschmidt amekosoa misimamo ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ya baadhi ya nchi za Magharibi na kusema: "Misimamo isiyo na mantiki ya madola kama Marekani imeibua migogoro mikubwa ya kisiasa, kiusalama na kijeshi katika upeo wa dunia na kuandaa mazingira yanayohatarisha amani na usalama wa kimataifa."

Bertrand Goldschmidt

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 28 Oktoba ilipendekeza muswada wa unaozitaka nchi wanachama katika mkataba wa kuzuia silaha za nyuklia wa NPT kuharibu silaha zao za nyuklia. Muswada huo ulipasishwa na akthari ya wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu. 

Teknolojia ya nyuklia inapewa mazingatio makubwa na nchi nyingi duniani kutokana na matumizi yake katika nyanja mbalimbali za viwanda, tiba na nishati safi. Iran kama zilivyo nchi nyingine, imetumia uwezo wa wasomi na wataalamu wake wa ndani kwa ajili ya kukamilisha mfumo wa kuzalisha fueli ya nyukliia, kupata teknolojia ya kisasa zaidi, kuzalisha nishati hiyo na kutumia mionzi ya nyuklia katika sekta ya kilimo, viwanda, matibabu na kadhalika na imepiga hatua kubwa katika nyanja zote hizo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliithibitishia dunia uwezo wake kubwa wa teknolojia ya nyuklia kwa kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20 katika kipindi kifupi sana.

Kwa sasa kinu cha utafiti wa nyuklia cha Tehran kinatumia sahani za fueli nyuklia zilizotengenezwa katika Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI). Vilevile kuongezeka kwa kiwango cha urutubishaji wa madini ya urani ni kielelezo cha uwezo na maendeleo ya kiteknolojia ya Jamhuri ya Kiislamu. Kuimarisha shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani kunafanyika kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa na Bunge la Iran Disemba mwaka jana. Siku hiyo wabunge wa Iran walipasisha kwa kishindo sheria inayofahamika kama "Mpango wa Kistratajia wa Kukabiliana na Vikwazo", na kuziagiza mamlaka husika za serikali kuchukua hatua zaidi za kupunguza uwajibikaji wa Iran katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Tangu wakati huo Iran iliainza kurutubisha madini ya urani kwa asilimia 60. Urani iliyorutubishwa kwa kiwango hicho inatumiwa kwa ajili ya kutengeneza aina mbalimbali za dawa za nyuklia.

Katika hatua hizo zote Iran imefuata na kuheshimu kikamiliifu mkataba wa kuzuia silaha za nyuklia na kanuni za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Katika mkondo huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba, Jamhuri ya Kiislamu haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia na kwamba shabaha yake kuu ni kupata teknolojia ya kisiasa na ya masuala ya amani ya nishati hiyo.

Ayatullah Ali Khamenei

Amesema kuuambia mkutano wa wasomi wenye vipawa nchini kwamba: "Elimu na sayansi inapojitenga na utamaduni sahihi hupoteza mwelekeko. Sayansi na teknolojia yenye manufaa mengi ya nyuklia ilipoteza njia na kuelekea kwenye uzalishaji wa kombora la nyuklia pale ilipoachana na utamaduni sahihi wa kibinadamu na hii leo imekuwa tishia kwa dunia. Tunaamini kwamba ni makosa kutengeneza na kumiliki silaha za nyuklia kwa sababu ni haramu kutumia silaha hizo."