Amir Abdullahiyan: Inawezekana kufikia mapatano na Wakala wa IAEA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema inawezekana kufikia mapatano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Hussein Amir Abdullahiyan ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa twitter kuhusu mazungumzo kati yake na Rafel Grossi Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kwa kusema: 'Mjini Tehran tumefanya mazungumzo ya kirafiki, ya wazi na yenye manufaa kati yangu na Rafael Grossi.' Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa wameafikiana vyema pia kuhusu kuendeleza ushirikiano wa pande mbili lakini kwamba uhitimishaji wa jambo hilo unahitajia kazi ya ziada.
Amir Abdullahiyan juzi Jumane alikutana na kufanya mazungumzo na Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kwa dhati kuendeleza ushirikiano na wakala huo katika fremu ya makubaliano yaliyofikiwa na pande mbili. Amesema anataraji kuwa hali ya kuaminiana na ushirikiano wa pande mbili utaimarishwa kupitia ziara hiyo ya Grossi hapa Tehran.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa IAEA amesisitiza kuhusu utendaji wa kiufundi, kitaaluma na usioegemea upande wowote wa wakala huo na kuitaja safari yake hapa Tehran kuwa ni ishara ya dhamira njema aliyonayo ya kuendeleza mazungumzo na uelewa wa pamoja, kutatua kadhia mbalimbali na kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.