Dec 07, 2021 14:13 UTC
  • Shamkhani: Marekani inataka kulifufua kundi la ISIS

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema Marekani ilighadhabishwa mno na kitendo cha kusambaratika kwa kundi la kigaidi la ISIS katika nchi za Syria na Iraq, na hivi sasa linafanya juu chini kulifufua genge hilo ili kuzusha mgogoro mpya katika eneo.

Ali Shamkhani amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Miqdad na kuongeza kuwa, kuibua mgogoro mpya nchini Syria ni njama iliyopikwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Amelaani wimbi la mashambulio yanayofanywa na utawala haramu wa Israel katika ardhi ya Syria na kubainisha kuwa, hujuma hizo ni muendelezo wa uvamizi haramu na katili wa Wazayuni dhidi ya Palestina na Lebanon.

Admeri Shamkhani ameeleza bayana kuwa, suala la kulifufua genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh ndilo lengo la kistratijia la Marekani, kwani inaamini kwamba genge hilo ni turufu ya kufanikisha malengo yake haramu katika eneo hili.

Shamkhani akimpokea ofisini kwake Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran kadhalika ameashiria kuimarika uhusiano wa kistratajia wa Jamhuri ya Kiislamu na Syria katika nyuga za usalama na siasa na kueleza kuwa, kuna haja ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga nyinginezo kama uga wa uchumi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Miqdad kwa upande wake amesema uwepo wa Marekani nchini Syria ni kinyume cha sheria na unakanyaga mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu. Amesema Washington inataka kuhuisha magenge ya kigaidi Syria.

Tags