Iran yakosoa azimio la haki za binadamu lililoungwa mkono na Canada
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78176-iran_yakosoa_azimio_la_haki_za_binadamu_lililoungwa_mkono_na_canada
Afisa wa ngazi za juu wa Idara ya Mahakama ya Iran amekosoa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo lilipitishwa hivi karibuni kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran na kusema, azimio hilo ambalo limeungwa mkono na Canada, ni la kisiasa, na halijazingatia uhalisia wa mambo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 18, 2021 13:09 UTC
  • Kazem Gharibabadi
    Kazem Gharibabadi

Afisa wa ngazi za juu wa Idara ya Mahakama ya Iran amekosoa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo lilipitishwa hivi karibuni kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran na kusema, azimio hilo ambalo limeungwa mkono na Canada, ni la kisiasa, na halijazingatia uhalisia wa mambo.

Kazem Gharibabadi, Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Idara ya Mahakama ya Iran ambaye pia ni Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran amesema azimio hiyo limetayarishwa na nchi ambayo ni moja kati ya wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu na limejaa madai yaisiyo na msingi na yaliyo mbali na uhalisi wa mambo.

Azimio hilo lilipasishwa Alhamisi iliyopita kwa kura 78 za kuunga mkono, 31 za kupinga huku nchi zingine 69 zikijizuia kupiga kura. Azimio hilo linatoa tuhuma dhidi ya Iran kuwa eti inakiuka haki za binadamu.

Gharibabadi amezilaani baadhi ya nchi za Magharibi kwa kujaribu kuidhihirisha Iran kama mkiukaji wa haki za binadamu.

Eneo kulikofanyika mauaji ya umati ya watoto wa jamii asilia za Canada

Aidha amesema nchi za Magharibi zinazotoa tuhuma dhidi ya Iran zenyewe ni wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu hasa haki za wakimbizi na wahajiri.

Gharibabadi ametoa mfano wa Canada na kusema nchi hiyo ni mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Amesema kwa mfano Wairani laki nne waishio Canada wamenyimwa huduma za kibalozi kutokana na kutokuwepo uhusiano wa kisiasa baina ya Tehran na Ottawa. Aidha amesema utawala wa Canada umekiuka haki za jamii za watu asili wa nchi hiyo ambapo hivi karibuni kumefichuka mauaji ya umati ya watoto wa jamii hizo katika shule zilizokuwa zikisimamiwa na Kanisa Katoliki.