Brigedia Jenerali Qaani: Shahid Irlu alikuwa mtumishi wa wananchi wanaodhulumiwa wa Yemen
(last modified Tue, 21 Dec 2021 11:54:30 GMT )
Dec 21, 2021 11:54 UTC
  • Brigedia Jenerali Esmail Qaani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH
    Brigedia Jenerali Esmail Qaani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, shahid Hasan Irlu, balozi wa Iran nchini Yemen ambaye amefariki dunia kwa ugonjwa wa corona, alikuwa mtumishi wa wananchi madhulumu na wanamuqawama wa Yemen.

Brigedia Jenerali Esmail Qaani amesema hayo leo katika ujumbe alioutoa wa kupongeza na kutoa mkono wa pole kufuatia kufa shahidi kwa corona Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Yemen na kusisitiza kuwa, huduma zilizojaa baraka zilizotolewa na shahid huyo katika miaka yote iliyopita, ni ukurasa wa dhahabu kwenye historia ya Mapinduzi ya Kisilamu hususan katika miaka ya hivi karibuni alipoteuliwa kuwa balozi wa Iran nchini Yemen.

Amesema, shahid Irlu amefanya kazi kubwa ya kuwapunguzia mateso wananchi wanaodhulumiwa wa Yemen na ameacha kumbukumbu nzuri ya kuwatumikia wananchi madhulumu wa Yemen, kuwa karibu nao na kujitahidi kadiri alivyoweza kuwatatulia matatizo yao.

Shahid Hasan Irlu, aliyekuwa Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Yemen

 

Kabla ya hapo Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alikuwa ametangaza kupitia ujumbe maalumu kwamba Balozi wa Iran nchini Yemen Bw. Hasan Irlu amekufa shahidi kwa ugonjwa wa UVIKO-19.

Shahid Hasan Irlu alikuwa majeruhi wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya 1980. Alipata ugonjwa wa corona wakati alipokuwa anawatumikia wananchi wa Yemen. Alirejea hapa Iran akiwa na hali mbaya na leo Jumanne amekufa shahidi kwa ugonjwa huo.

Viongozi mbalimbali wa humu nchini na wa Yemen akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu Iran wametoa mkono wa pole kwa kumpoteza mwanamuqawama huyo.