Jan 03, 2022 02:32 UTC
  • Shahidi Qassem Soleimani na kuimarisha na kuinua nafasi ya muqawama Asia Magharibi

Moja ya maudhui muhimu kuhusiana na Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ni mchango wake katika kuimarisha na kuinua nafasi ya muqawama na mapambano katika eneo la Asia Magharibi.

Vita dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, chuki dhidi ya ubeberu, kupinga udikteta, chuki dhidi ya dhulma, kupigania uadilifu, haki, amani, izza, heshima, nguvu, mamlaka ya kujitawala, kuwa na muelekeo wa kimaanawi na kuzingatia maslahi ya wananchi ni miongoni mwa vielelezo muhimu vya harakati ya muqawama katika eneo la Asia Magharibi.

Katika muongo mmoja wa hivi karibuni, mhimili wa muqawama siyo tu kwamba, umeendesha harakati ya kuhakikisha unabakia, bali umeweza kujiimarisha na kuinua nafasi na kiwango chake cha nguvu na uwepo wake katika eneo, kama ambavyo umefanya mambo ili kuhakikisha unafikia vigezo  vyake hivyo. Kimsingi ni kuwa, katika muongo mmoja uliopita, maadui wamekuwa na utendaji wa kufanya hujuma mkabala na muqawama huku mhimili huu ukiwa na utendaji wa kujihami mbele ya maadui.

Marekani pamoja na washirika wake wa Kiarabu na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel walianzisha njama za kuidhoofisha Syria mwaka 2011huku wakiota ndoto za kutaka kubadilisha utawala katika nchi hiyo ya Kiarabu inayoongozwa na Rais Bashar al-Assad aliyechaguliwa kihalali na kwa njia ya demokrasia. 

Mashahidi Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis

Sababu ya kuichagua Syria ni kutokana na kuwa, nchi hiyo imo katika mduara wa mhimili wa muqawama na njama za Marekani na waitifaki wake zililenga kusambaratisha mhimili huu. Kile ambacho tunakishuhudia leo hii baada ya kupita muongo mmoja tangu kuanza njama hizo ni kuimarika na kupata nguvu mhimili wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi ambapo Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa na nafasi muhimu na kubwa na kwa namna fulani ndiye aliyekuwa nafasi kuu katika kupatikana matunda haya.

Hussein Kan'an Moqaddam mwanaharakati wa kisiasa na mmoja wa makamanda waandamizi na wa zamani wa jeshi la Sepah anasema: Moja ya sifa za kipekee za Luteni Jenerali Soleimani, ni kipaji cha hali ya juu cha masuala ya kijeshi na kuwa na fikra pana na upeo wa hali ya juu wa kistratejia.

Mark Hertling jenerali mstaafu wa jeshi la kigaidi la Marekani na mchambuzi wa masuala ya usalama wa taifa, ujasusi na ugaidi naye anasema kuwa, Soleimani alikuwa na kipawa cha kistratejia na kamanda mwenye mikakati na mbinu.

Hapana shaka kuwa, kipawa hiki cha masuala ya kijeshi ndicho kilichomjenga Shahidi Qassem Soleimani na kumfanya kuwa kamanda wa ushindi.

Shahidi Qassem Soleimani enzi za uhai wake akiteta jambo la Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Hatua yake ya kuweko nchini Syria na kuyapanga vyema makundi ya muqawama katika nchi hiyo ilizuia magaidi na washirika wao wa pande nne yaani mhimili wa Kimagharibi-Kiarabu-Kiibrania na Kituruki kufikia malengo yao katika jiografia ya Syria. Hii leo siyo tu kwamba, muqawama umeweza kulinda na kuhifadhi ardhi ya Syria, bali mfumo wa kisiasa wa Damascus unatembea kifua mbele mkabala wa magaidi ambao wamedhoofika mno na kutokuwa na uwezo wa kufanya kitu.

Maadui wa muqawama wakiwa na lengo la kutoa pigo dhidi ya mhimili huu walitumia mbinu ya kuenea ugaidi katika mataifa mengine ya jirani na muqawama ikiwemo Iraq.

Ukweli wa mambo ni kuwa, maadui walifanya njama za kuhakikisha kwamba, ugaidi hauishii katika jiografia ya Syria tu, bali unavuka mipaka na kuingia katika nchi kama Lebanon, Iraq na hata Iran. Moja ya stratejia za Shahidi Qassem Soleimani za kukabiliana na kusambaratisha njama hiyo ya maadui ni kuratibu na kuunganisha pamoja nguvu za muqawama.

Katika fremu ya stratejia ya kuratibu na kuunganisha pamoja nguvu za muqawama, kukatokea mfungamano wa kijiografia baina ya wanachama wa mhimili huu katika mataifa mbalimbali. Matokeo ya mkakati huu ni kuwahami na kuwalinda wanachama wa muqawama hususan Syria na Iraq.

Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani

 

Kimsingi ni kuwa, shahidi wa muqawama Luteni Jenerali Qassem Soleimani akiwa kamanda mahiri wa muqawama akiwasaidia makamanda wengine wa mhimili huu aliweza kuunganisha pamoja mnyonyoro wa mhimili wa muqawama na kama alivyosema Brian Katz mwananadharia mwenye ukuruba na Ikulu ya White House ni kuwa, kwa hatua yake hiyo Qassem Soleimani akawa ameunda jiopolitiki ya muqawama.

Mkakati huu umekuwa na matokeo mengi ambapo miongoni mwayo ni kushindwa vibaya ugaidi wa Kidaesh na makundi mengine ya kigaidi katika nchini za Syria na Iraq na kuzuia vita vya kigaidi nchini Syria kuenea katika nchi za Lebanon na hata Iran na kuyafanya makundi ya muqawama kuwa, harakati ya wananchi yenye taathira muhimu katika medani ya kisiasa na kiusalama katika mataifa ya Syria, Iraq na Lebanon.

Hali hii baada ya kupita muongo mmoja wa njama dhidi ya muqawama, imeufanya mhimili huu uzidi kuimarisha na kuboresha nafasi yake katika uga wa kieneo ambapo hakuna shaka kwamba, moja ya sababu za mafanikio haya ni kipaji cha kistratejia chenye sifa za kamanda wa kweli cha shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Tags