Ravanchi: Utawala wa Syria haupaswi kudhoofishwa kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80778-ravanchi_utawala_wa_syria_haupaswi_kudhoofishwa_kwa_kisingizio_cha_kupambana_na_ugaidi
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, kuwepo kinyume cha sheria majeshi ya kigeni katika baadhi ya maeneo ya Syria kumetayarisha mazingira ya harakati na shughuli za makundi ya kigaidi nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 26, 2022 07:47 UTC
  • Majid Takht-Ravanchi
    Majid Takht-Ravanchi

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, kuwepo kinyume cha sheria majeshi ya kigeni katika baadhi ya maeneo ya Syria kumetayarisha mazingira ya harakati na shughuli za makundi ya kigaidi nchini Syria.

Majid Takht-Ravanchi amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ugaidi hayawezi kutumika kama kisingizio cha kudhoofisha mamlaka na ardhi ya Syria.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ambaye jana Ijumaa alikuwa akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la UN kuhusu hali ya kisiasa na kibinadamu nchini Syria, ameashiria ukiukaji wa mara kwa mara wa utawala wa Israel wa mamlaka ya nchi hiyo na kusema: Mashambulizi ya karibuni ya utawala haramu wa Israel nchini Syria, ambayo yamelenga raia na miundombinu ya kiraia, ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Amesema Iran inatoa wito kwa Baraza la Usalama kuuwajibisha utawala huo wa Israel kwa vitendo hivyo vya uchokozi na viovu, pamoja na vitisho vyake vya kutumia nguvu dhidi ya mataifa mengine katika eneo la Magharibi mwa Asia, jambo ambalo linahatarisha amani na usalama wa eneo hilo. 

Amesema mamlaka ya Syria inaendelea kukiukwa kutokana na uvamizi wa majeshi ya nchi za kigeni yakiwemo majeshi ya Marekani na kuongeza kuwa: "Tunalaani wizi wa maliasili za watu wa Syria katika maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya kigeni, hususan mafuta na mazao ya kilimo, na tunatambua haki halali ya serikali ya Syria kupambana na vitendo hivyo vya uhalifu."

Magari ya jeshi la Marekani yakiiba mafuta ya Syria

Kwa mujibu wa serikali ya Syria, magaidi wa jeshi la Marekani na vibaraka wao huko mashariki na kaskazini mashariki mwa Syria wamekuwa wakipora mafuta ya nchi hiyo na kamba lazima askari hao waondoke katika eneo hilo haraka iwezekanavyo.