Duru mpya ya mazungumzo ya Iran na EU kuanza leo
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya leo Jumatatu zinatazamiwa kuanza duru mpya ya mazungumzo, ikiwa ni ya kwanza tangu Tehran na kundi la 5+1 kufikia makubaliano ya nyuklia ya Vienna mwaka jana.
Majid Takhte Ravanchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ambaye anasimamia masuala ya Ulaya na Amerika amesema mazungumzo hayo ya Iran na Umoja wa Ulaya yataanza leo kwa kuwashirikisha wajumbe wa Iran na umoja huo wakiongozwa na Helga Schmid, Naibu Mkuu wa sera za nje wa EU. Mwanadiplomaisa huyo wa Iran amesema mazungumzo hayo ya kiwango cha manaibu, yatajikita zaidi katika masuala ya nishati, biashara, ushirikiano wa kifedha na kibenki, mazingira na vita dhidi ya mihadarati.
Kadhalika Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema masuala ya kieneo na hususan mgogoro wa Syria, Iraq na Yemen pia yamo katika ajenda ya mkutano huo.
Itakumbukwa kuwa, makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama JCPOA yalisainiwa mwezi Julai mwaka jana na kuanza kutekelezwa Januari 16 mwaka huu.