Iran yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Wamarekani wanaohusika na ugaidi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza orodha mpya ya vikwazo dhidi ya raia wa Marekani wanaohusika na vitendo vya ugaidi na ukiukaji wa haki za binadamu.
Taarifa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: "Katika fremu ya utekelezaji wa sheria ya kukabiliana na ukiukaji wa haki za binadamu, ugaidi na chokochoko za Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia, majina mapya ya Wamarekani yanaongezwa katika orodha ya watu wanaowekewa vikwazo na Iran kutokana na kuhusika kwao katika vitendo vya ugaidi, kuhimiza na kuunga mkono ugaidi na ukiukwaji wa haki za binadamu."
Taarifa hiyo imesema, Wamarekani walio katika orodha hiyo wamehusika pia katika kupanga, kuunga mkono na kushadidisha vikwazo vya upande mmoja na vya kijinai vya Marekani dhidi ya taifa la Iran. Aidha Wamarekani hao ambao Iran imewawekea vikwazo wamehusika katika kuyafadhili kifedha makundi ya kigaidi na pia wamepatikana na hatia ya kuunga mkono vitendo vya ukandamizaji vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia hasa dhidi ya taifa madhulumu la Palestina.

Utawala wa Marekani pia umekuwa ukichukua hatua za upande mmoja na za makusudi kwa lengo la kuyafanya maisha ya Wairani yawe magumu kupitia kuzuia hatua za dawa muhimu kuingia nchini na pia kuizuia Iran kupata vifaa vya tiba hasa wakati huu wa janga la COVID-19. Uhasama huo wa Marekani umehatarisha maisha ya mamilioni ya Wairani na kuwazuia kupata haki za kiuchumi na kijamii.
Taarifa hiyo imesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua uamuzi za kuweka vikwazo dhidi ya raia hao wa Marekani katika utekelezaji wa majukumu yake ya kimataifa ya haki za binadamu na kupambana na ugaidi, hasa mapambano dhidi ya ugaidi wa Marekani.