Iran yawaasa Waislamu duniani waungane kuwatetea Wapalestina, Msikiti wa Aqsa
(last modified Sun, 17 Apr 2022 03:26:15 GMT )
Apr 17, 2022 03:26 UTC
  • Iran yawaasa Waislamu duniani waungane kuwatetea Wapalestina, Msikiti wa Aqsa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa mara nyingine tena amelaani jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuushambulia na kuuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa na kusisitiza kuwa, mataifa ya Kiislamu yanapaswa kuungana na kusima bega kwa bega kuitetea kadhia ya Palestina.

Saeed Khatibzadeh alitoa mwito huo jana Jumamosi katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa: Kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa kibaguzi wa Israel hakuna matokeo mengine ghairi ya kumshajiisha dhalimu ashadidishe ukatili wake maradufu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, Waislamu kote duniani sharti waungane kuwatetea wananchi wa Palestina na kuuhami Msikiti mtakatifu wa al-Aqsa.

Khatibzadeh ameuabatanisha ujumbe wake na ujumbe wa Sheikh Ikrima Sabri, Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu Quds ambaye pia amekosoa na kukitaja kama fedheha, kimya cha nchi za Kiislamu mkabala wa kuvunjiwa heshima Masjidul Aqsa.

Maghasibu wa Kizayuni juzi Ijumaa kwa mara nyingine tena waliushambulia na kuhujumu Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa ambacho ni Kibla cha kwanza cha Waislamu na kuibua mapigano kati yao na Wapalestina.

Askari vamizi wa Israel wakiwashambulia Waislamu nje ya Masjidul Aqsa

Wapalestina zaidi ya 220 walijeruhiwa na wengine 400 walitiwa nguvuni na wanajeshi wa Israel. Wapalestina 17 wameuliwa shahidi tangu siku 15 zilizopita hadi kufikia jana Jumamosi. 

Siku ya Ijumaa, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliashiria uvamizi huo dhidi ya Aqsa na kusisitiza kuwa, utawala haramu wa Israel umekiuka wazi wazi misingi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa kwa chokochoko zake hizo.