Marais wa Iran na Indonesia wasisitiza kupanua uhusiano katika nyanja mbalimbali
(last modified Thu, 05 May 2022 02:44:44 GMT )
May 05, 2022 02:44 UTC
  • Marais wa Iran na Indonesia wasisitiza kupanua uhusiano katika nyanja mbalimbali

Marais wa Iran na Indonesia wamefanya mazungumzo ya simu wakijadili uwezo wa nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali na kusisitiza ulazima wa kufanyika juhudi za pamoja za kuboresha kiwango cha ushirikiano wa pande mbili.

Ayatullah Sayyid Ebrahim Raisi jana Jumatano alimpongeza Rais wa Indonesia, Joko Widodo na wananchi wa nchi yake kwa mnasaba wa sherehe za Idul Fitr na kueleza matumaini yake kuwa, kwa baraka za sikukuu hiyo kubwa taifa na serikali ya Indonesia na mataifa yote ya dunia yatafanikiwa kuishi katika hali ya amani na usalama.

Akizungumzia nafasi mbalimbali zilizopo katika nchi hizo mbili, Raisi ameongeza kuwa: "Uhusiano kati ya Iran na Indonesia unaweza kupanuliwa zaidi katika nyanja zote kwa kufanya kazi pamoja."

Ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuboresha uhusiano wake wa kikanda na kimataifa kwa kutoa kipaumbele zaidi kwa nchi marafiki.

Akizungumzia umuhimu wa suala la Palestina katika ulimwengu wa Kiislamu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Nchi za Kiislamu zinapaswa kuwa na mshikamano na umoja katika kutetea mapambano ya watu wa Palestina."

Kwa upande wake, Rais Joko Widodo wa Indonesia amempongeza Rais na wananchi wa Iran kwa sikukuu ya Idul Fitr na kusisitiza nia ya nchi yake ya kutaka kuendeleza ushirikiano wa pande mbili, kieneo na kimataifa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika uga wa nishati na afya. 

Rais wa Indonesia amesema: Mbali na masuala yanayozikutanisha pamoja ya kiutamaduni, Iran na Indonesia pia zina mitazamo inayokaribiana kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa, na zote zinaunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina.