Abdollahian: Iran inapinga vita vya Ukraine na eneo lolote duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i83402
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuna wajibu wa kufanyika mazungumzo ya kisiasa baina ya Ukraine na Russia kwa ajili ya kukomesha haraka vita huko Ukraine kwani vita si kwa manufaa ya upande wowote.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 09, 2022 02:21 UTC
  • Abdollahian: Iran inapinga vita vya Ukraine na eneo lolote duniani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuna wajibu wa kufanyika mazungumzo ya kisiasa baina ya Ukraine na Russia kwa ajili ya kukomesha haraka vita huko Ukraine kwani vita si kwa manufaa ya upande wowote.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumapili mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Poland, Zbigniew Rau na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vita vya Ukraine na eneo lolote lile duniani.

Amesema, kama ambavyo Iran inapinga vita katika nchi za Iraq, Afghanistan, Yemen na Syria, inapinga vita pia huko Ukraine na sehemu nyingine yoyote na inaamini kuwa, njia pekee ya kuweza kutatua mgogoro wa Ukraine ni ya kisiasa na inabidi mazungumzo ya kisiasa yafanyike haraka ili kusimamisha vita mara moja huko Ukraine.

Wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Ukraine

 

Amesema, mara tu baada ya kuanza vita vya Ukraine, alizungumza kwa simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Poland na kutangaza kuwa Tehran iko tayari kupeleka timu ya madaktari 25 wa kutibu majeruhi na wagonjwa katika mpaka wa Ukraine na Poland na pia kupeleka huko misaada ya kibinadamau. Lakini kwa vile Shirika la Msalaba Mwekundu lilikuwa limeshaweka timu yake ya madaktari kwenye eneo hilo, haikuwezekana tena kwa Iran kupeleka timu yake ya madaktari.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Zbigniew Rau, aliwasili hapa Tehran usiku wa kuamkia jana akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa nchi yake kwa ajili ya ziara rasmi ya kikazi na kwa ajili ya kuonana na kuzungumza na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala tofauti ya pande mbili na ya kimataifa.