Jun 12, 2022 07:57 UTC
  • Kundi la kwanza la mahujaji wa Kiirani laondoka nchini kwenda Saudia

Kundi la kwanza la wananchi wa Iran wanaokwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija limeondoka nchini mapema leo Jumapili kwenda katika mji mtukufu wa Madina nchini Saudi Arabia.

Sayyid Sadeq Hosseini, Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria miongozo iliyotolewa hapo awali na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu Hija ya mwaka huu na kusema kuwa, jumla Wairani 39,635 watakwenda kutekeleza ibada hiyo tukufu mwaka huu, wakitokea kwenye viwanja 17 vya ndege vya Jamhuri ya Kiislamu.

Mahujaji hao wote ni wale waliotimiza masharti yaliyoainishwa, yakiwemo ya kupiga chanjo kamili za kujikinga na ugonjwa hatari wa Corona (Covid-19). Mahujaji 1,300 wameondokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kerman, kusini mashariki mwa Iran, Tabriz, kaskazini magharibi na wengine wakitokea katika Uwanja wa Kimataifa wa Imam Khomeini hapa jijini Tehran.

Saudi Arabia ilitangaza kuwa itawaruhusu Waislamu milioni moja kutoka ndani na nje ya nchi kushiriki katika Hija mwaka huu, hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi baada ya vizuizi vya janga la Corona kulazimisha kupunguzwa idadi ya mahujaji katika kipindi cha miaka miwili mfululizo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian katika ujumbe aliotuma mapema leo kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, mbali na kuzitakia ufanisi taasisi husika za Saudia katika kusimamia Hija mwaka huu, ametoa mwito wa kuhakikisha kuwa amali za nguzo hiyo ya Kiislamu zinafayika kwa usalama, amani, hadhi ya juu na umoja.

Hija kwa kawaida huwa  moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini ulimwenguni, ambapo mwaka 2019 takriban Waislamu milioni 2.5 walishiriki katika ibada hiyo.

Tags