Kiongozi Muadhamu ataja vipaumbele vya Bunge la Iran
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, uchumi wa kimuqawama, utamaduni na kufuatilia siasa za ndani ya nchi, za kieneo na za kimataifa ndivyo vipaumbele vikuu vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).
Ayatullah Khamenei amesema hayo leo Jumapili wakati alipoonana na Spika na wabunge wa Bunge la 10 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na huku akitilia mkazo wajibu wa kulindwa nguvu na nafasi ya Bunge kikiwa ni chombo kikuu kinachosimamia masuala ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, amesisitiza kuwa, mbali na Bunge kuwa na wajibu wa kupuliza roho ya utulivu nchini, lina wajibu pia wa kutunga sheria kimapinduzi na kuchukua msimamo thabiti mbele ya uadui wa Marekani kama ambavyo lina wajibu pia wa kusimama kidete kukabiliana na siasa za mabeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu wana nafasi muhimu sana katika ufanikishaji wa siasa za uchumi wa kimuqawama kwani wana uwezo wa kubadilisha mwelekeo wa hatua za kiuchumi za Serikali na kuzielekeza upande wa uchumi wa kimuqawama na kuitaka serikali ifuate msimamo huo.
Ayatullah Khamenei aidha amesisitiza kuwa, adui anaendesha njama maalumu dhidi ya eneo muhimu na nyeti la magharibi mwa Asia na anafanya kila awezalo kuhakikisha anazivunja siasa za Iran ambazo ni kizuizi katika ufanikishaji wa njama zake za kiuadui.
Kiongozi Muadhamu amesema pia kuwa, njama za Marekani zimeshindwa katika nchi kama za Iraq, Syria, Lebanon na pia Palestina kutokana na kusimama imara Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, kuna wajibu wa kusimama kidete kukabiliana na siasa za kiistikbari na kufichua ubeberu wao.