Jun 06, 2016 07:23 UTC
  • Rouhani: Inachotaka Iran ni kuona amani na uthabiti katika eneo

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema fahari ya Jamhuri ya Kiislamu ni kuona amani na uthabiti vinatamalaki katika eneo la Mashariki ya Kati.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana jioni katika mkutano na Edward Nalbandian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Iran imekuwa ikifanya juu chini kuhakikisha kuwa changamoto na migogoro katika nchi za eneo hili inapatiwa ufumbuzi kwa njia za amani. Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haitachoka kuendeleza jitihada zake za kuona kuwa eneo hili linakuwa pahala penye amani, usalama na uthabiti na kusisitiza kuwa, kuimarisha uhusiano miongoni mwa nchi za eneo, kutatoa mchango mkubwa katika kufanikisha hilo. Wakati huo huo, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili kati ya Tehran na Yerevan katika nyuga za uchumi, utamaduni, utalii, biashara, kilimo na uchukuzi, haswa katika kipindi hiki cha kutekelezwa Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kati ya Iran na madola 6 yenye nguvu duniani.

Kwa upande wake, Edward Nalbandian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia amesema licha ya Yerevan na Tehran kuwa na historia pana ya kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri lakini kuna haja ya kuimarishwa mahusiano hayo katika sekta mbali mbali. Mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Hassan Rouhani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Armenia amekutana na mwenzake wa Iran Muhammad Javad Zarif na Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) Ali Larijani na kubadilishana naye mawazo juu ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Tags