Iran yajibu hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo vipya
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo vipya Jamhuri ya Kiislamu licha ya kudai kiuongo kuwa inataka yafanikiwe mazungumzo ya kuondolewa vikwazo Iran kupitia mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Jana Jumatatu, Wizara ya Hazina ya Marekani iliyawekea vikwazo mashirika mengine mapya kwa madai ya kuwa na ushirikiano na Iran. Mashirika hayo yako katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), China, Singapore na Malaysia.
Marekani ndiyo nchi yenye uraibu mkubwa zaidi wa kuweka vikwazo duniani. Inatumia vikwazo kama njia ya kufanikishia malengo yake haramu dhidi ya nchi nyingine.
Shirika la habari la Fars limemnukuu Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akisema mapema leo Jumanne kwamba, itibari ya Marekani inazidi kuharibika kutokana na uraibu wake wa kuziwekea vikwazo nchi nyingine.
Amesema, hatua hiyo inazidi kuonesha sifa ya kibeberu ya Washington na tabia yake ya kutumia mabavu kupinduwa tawala zilizochaguliwa kidemokrasia za nchi nyingine duniani.
Aidha amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwanza itatoa majibu makali na haraka dhidi ya hatua ya Marekani ya kuendelea kuweka vikwazo vyake kiholela na pili itachukua hatua zote zinazotakiwa kwa ajili ya kufelisha vikwazo hivyo kama ambavyo taifa hili la Kiislamu limekuwa likifanya kwa zaidi ya miongo minne sasa na kufanikiwa kusimama imara mbele ya mashinikizo hayo.