Aug 05, 2022 12:24 UTC
  • Hujjatul Islam Akbari: Imam Hussein aliarifisha wazo la 'Muqawama' kwa waumini

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema Imam Hussein (AS) aliarifsha hoja ya muqawama kwa waumini wote wa Kiislamu, na kwamba mapambano ndiyo njia pekee ya kupata mafanikio.

Hujjatul Islam Haj Ali Akbari amesema hayo katika hotuba za Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa Tehran na kubainisha kuwa, "Kile ambacho Imam Hussein (AS) alikifanya kilikuwa kitu cha kipekee, kwa kuutambulisha muqawama kwa jamii ya waumini."

Haj Ali Akbari ameeleza bayana kuwa, hii leo harakati za muqawama wa Kiislamu katika pembe mbalimbai za dunia zimebaki hai kutokana na kujitoa muhanga Imam Hussein (AS).

Imam Hussein (AS) ambaye kwa kujitolea kwake mhanga kusio na kifani aliuawa shahidi Siku ya Ashura, yaani tarehe 10 Muharram katika ardhi ya Karbala, amewaachia walimwengu wote somo kubwa la maana halisi ya kukomboka na kuwa na izza na heshima.

Katika sehemu nyingine ya hotuba zake, Imam huyo wa muda wa Swala ya Ijumaa hapa Tehran amebainisha kuwa, maafisa wa serikali ya Iran hawajaufungamanisha uchumi wa taifa hili na mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo haramu.

Amesisitiza kuwa, timu ya mazungumzo ya Iran itayalinda maslahi ya taifa hili kwa nguvu zote, na kueleza kwamba, "Tunatoa mwito kwa maadui, Marekani na washiriki wengine wa mazungumzo wasithubutu kuipa Iran mtihani. Iwapo mnahitaji kufanya mazungumzo, tekelezeni masharti ya Iran na muache kujipendea makuu." 

Tags