Waislamu Iran, Nigeria waungana na wenzao kote duniani katika maombolezo ya Ashura
(last modified Mon, 08 Aug 2022 07:33:49 GMT )
Aug 08, 2022 07:33 UTC
  • Waislamu Iran, Nigeria waungana na wenzao kote duniani katika maombolezo ya Ashura

Wananchi Waislamu hapa Iran na Nigeria jana na leo wameungana na mamilioni ya wafuasi wengine wa Ahlul-Baiti (as) duniani kote katika kumbukumbu ya mauaji ya mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS.

Waombolezaji katika Iran ya Kiislamu, leo wanashiriki kwenye majlisi za maombolezo kukumbuka ushujaa na dhulma waliotendewa mashahidi wa Karbala, miaka 1383 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria.

Matabaka tofauti ya wananchi Waislamu wa Iran wakiwemo vijana na wazee, wake kwa waume wameghariki kwenye dimbwi la huzuni na maombolezo ya Ashura, ya kukumbuka siku aliyouliwa shahidi Imam Hussein AS katika ardhi ya Karbala.

Waislamu nchini Iran na maeneo mengine ya dunia hapo jana tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram walishiriki katika vikao, majlisi na shughuli za maombolezo ya Tasua.

Habari zaidi zinasema kuwa, hafla za maombolezo ya Ashura mwaka huu huko Nigeria zinafanyika katika majimbo karibu yote ya kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Aidha maombolezo ya Imam Hussein AS yanafanyika katika baadhi ya miji ya majimbo ya kusini mwa Nigeria.

Mwaka jana, askari polisi nchini Nigeria waliwashambulia waombolezaji katika kumbukumbu ya Ashura ya Imam Hussein (AS) na kuua na kujeruhi kadhaa miongoni mwao.

Ashura Nigeria

Mara kwa mara askari wa Nigeria wamekuwa wakishambulia waombolezaji wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.