Abdollahian awapongeza wanamuqwama kwa kukabiliana na wanajeshi wa Kizayuni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwa mara nyingine tena wanajihadi za harakati za muqawama wa Palestina wameweza kusimama kidete mkabala wa nguvu kubwa za kijeshi za utawala wa Kizayuni, na hatimaye wakawalazimisha maadui kusalimu amri na kuafiki kusitisha vita.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo ya simu na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na kuongeza kuwa, kitendo cha utawala haramu wa Israel kuafiki makubaliano ya usitishaji vita ni mafanikio makubwa kwa mrengo wa muqawama.
Ameeleza bayana kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni za kuwaua shahidi wanawake na watoto wa Kipalestina zinaonesha wazi udhaifu wa utawala huo pandikizi, na kasi kubwa ya kuporomoka kwake ambaio haijawahi kushuhudiwa tena.
Kwa upande wake, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema Wazayuni walijaribu kuwatwisha Wapalestina na wamuqawama wa Ukanda wa Gaza mahesabu yao ghalati, lakini wamekabiliwa na ushujaa wa muqawama wa Palestina.
Ijumaa ya tarehe 5 Agosti, ndege za utawala wa Kizayuni zilianzisha mashambulizi dhidi ya baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Gaza na vita hivyo vya siku tatu vimepelekea Wapalestina 45 kuuawa shahidi na wengine 360 kujeruhiwa wakiwemo wanawake na watoto wadogo.
Katika kujibu jinai hizo za Wazayuni, makundi ya muqawama ya Palestina yamevurumisha mamia ya makombora katika miji inayokaliwa na walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina ambazo zimepachikwa jina la Israel hasa Tel Aviv na Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion.
Utawala wa Kizayuni umejaribu kuficha hasara ambazo umepata kutokana na maroketi hayo ya Wapalestina. Haniya amesema ushindi huo wa mrengo wa muqawama umefungua ukurasa mpya katika vita vya mapambano ya Wapalestina dhidi ya adui Mzayuni.