Iran: Hatujapokea jibu la US kuhusu mapendekezo ya Ulaya
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haijapokea majibu kutoka kwa Marekani juu ya mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Ulaya kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Nasser Kan'ani amesema hayo leo Jumatatu hapa mjini Tehran katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari na kueleza kuwa, Marekani inajichelewesha kutoa majibu kwa mapendekezo ya Ulaya.
Amesisitiza kuwa: Tutaweza kusema kuwa awamu hii ya mazungumzo imefanikiwa baada ya upande wa Ulaya kutangaza kuwa umepokea jibu kutoka Marekani.
Kan'ani ameeleza bayana kuwa, masuala yaliyosalia ni hasasi na yana umuhimu mkubwa, na kwa msingi huo sharti yafanyiwe maamuzi na yaafikiwe.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu haitasubiri daima upande pili, na kwamba katu haitafungamanisha ustawi wake wa kiuchumi na mazungumzo hayo ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu.

Siku chache zilizopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikabidhi kwa mratibu wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo hayo ya kuondolewa taifa la Iran vikwazo, jibu la maandishi la Tehran kuhusiana na nakala rasmi ya rasimu ya mapatano ya Vienna.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian hivi karibuni alisema: Ikiwa jibu la Marekani litaendana na uhalisia wa mambo na kuwa tayari kubadilika kulingana na hali, mwafaka utafikiwa; lakini kama Marekani haitaonyesha mabadiliko itabidi tufanye mazungumzo zaidi.