Iran yatangaza utayari wa kuwasaidia waathirika wa mafuriko Pakistan
(last modified Sun, 28 Aug 2022 07:48:15 GMT )
Aug 28, 2022 07:48 UTC
  • Iran yatangaza utayari wa kuwasaidia waathirika wa mafuriko Pakistan

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Iran iko tayari kutoa msaada wa aina yoyote kwa watu walioathiriwa na mafuriko katika nchi ndugu na jirani ya Pakistan.

Kufuatia mafuriko makubwa yaliyotokea siku za hivi karibuni katika maeneo makubwa ya Pakistan na kusababisha vifo vya watu takriban 1,000, serikali ya nchi hiyo imeyatangaza mafuriko hayo janga la kitaifa na kuomba msaada kwa nchi jirani na jumuiya ya kimataifa ili kuwasaidia waathirika wa janga hilo na kufidia pia uharibifu liliosababisha.
Rais Ebrahim Raisi, amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shahbaz Sharif, ambapo sambamba na kutoa salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Pakistan kutokana na watu waliopoteza maisha katika mafuriko yaliyotokea nchini humo hivi karibuni, amesisitiza kuendelea kwa uhusiano wa kirafiki na kindugu uliopo kati ya nchi mbili.
 
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, agizo limeshatolewa kwa taasisi zinazohusika ili misaada muhimu na ya msingi iweze kufikishwa haraka kwa wananchi azizi na waheshimika wa Pakistan, na akabainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa msaada wa aina yoyote kwa watu wa nchi ndugu na jirani ya Pakistan.
Mafuriko Pakistan

 

Kwa upande wake  Waziri Mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif ameelezea kiwango cha hasara, uharibifu na maafa yaliyosababishwa na mafuriko ya hivi karibuni nchini humo na  akatoa shukurani kwa misaada inayotolewa na serikali na wananchi wa Iran kwa watu wa Pakistan.
Waziri Mkuu wa Pakistan amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa jirani msaidizi, rafiki na nchi iliyo bega kwa bega na Pakistan katika nyakati ngumu.
Pakistan hushuhudia mvua za msimu kila mwaka, lakini mabadiliko ya tabianchi yanachangia kunyesha mvua kali ambazo zinasababisha mafuriko makubwa nchini humo.../