Raisi: JCPOA itafufuliwa kwa kusuluhishwa masuala yaliyosalia
(last modified Mon, 29 Aug 2022 11:29:17 GMT )
Aug 29, 2022 11:29 UTC
  • Raisi: JCPOA itafufuliwa kwa kusuluhishwa masuala yaliyosalia

Rais Ebrahim wa Raisi wa Iran amesema mapatano ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yatafikiwa tu kwa kupatiwa ufumbuzi masuala yaliyosalia baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.

Rais Raisi amesema hayo leo katika kikao na waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi hapa jijini Tehran na kusisitiza kuwa, pasi na kutatuliwa masuala yaliyosalia, makubaliano ya JCPOA hayatakuwa na maana yoyote.

Amesema, "Mazungumzo yanaendelea katika fremu hiyo na yanalenga zaidi juu ya suala la uondoaji vikwazo. Tunasisitiza kuhusu kupatiwa ufumbuzi kikamilifu masuala ya dhamana."

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitilia mkazo suala la kupewa dhamana kwamba Marekani haitajiondoa tena iwapo itaruhusiwa kurejea katika makubaliano ya JCPOA kama ilivyofanya mwaka 2018.

Sayyid Ebrahim Raisi ameashiria vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, hakuna mtu anayeweza kulizuia taifa la Iran kufidi na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani.

Rais Raisi

Amesema: Tumesisitiza mara kwa mara kwamba silaha za nyuklia hazina nafasi katika mafundisho ya dini yetu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (Ayatullah Ali Khamanei) ametangaza mara kadhaa kwamba silaha za namna hiyo zimekatazwa na mafundisho ya dini.

Kadhalika Rais wa Jamhuri ya Kiisamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, matatizo ya nchi hii yatapatiwa ufumbuzi kwa kutegemea uwezo wa ndani, na sio kwa kusubiri madola ajinabi yabadilishe mitazamo yao.