Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Kusimama imara; njia ya kukabiliana na maadui
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja ghasia na machafuko yaliyoenea katika maeneo mbalimbali hapa nchini kuwa ni mpango usio wa kawaida na wa fedheha wa adui mkabala wa maendeleo na harakati za ubunifu na kubwa za taifa la Iran na kwamba, njia ya kukabiliana na maadui ni kusimama imara.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema hayo Jumatano ya jana alipokutana na kuzungumza na mkuu na wajumbe wa duru mpya ya Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu na kusisitiza kuwa, katika matukio ya hivi karibuni nafasi na mchango wa adui umebainika wazi na kuwa dhahiri kwa kila mtu, hata kwa wachambuzi wa nchi ajinabi wasioegemea upande wowote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hivi sasa imebainika wazi na kikamilifu kuhusu vitendo vya adui kama vile vya kuendesha propaganda, kufanya kila njia za kuathiri fikra za waliowengi, kuibua hisia mbalimbali miongoni mwa jamii, kufanya uchochezi na hata kutoa mafunzo kuhusu namna ya kutengeneza mada za milipuko na kusababisha moto.
Sisitizo la Kiongozi Muadhamu juu ya kupangwa na kuratibiwa nje ya nchi fujo na ghasia za hivi karibuni hapa Iran linapata maana hasa kwa kutiliana maanani himaya na uungajii mkono rasmi wa Wamagharibi na vyombo vya habari vibaraka vinavyorusha matangazo yao kwa lugha ya Kifarsi kama Sauti ya Marekani (VOA) na Kanali za Satalaiti la Iran International ambavyo vyanzo vyao vya fedha ni madola ya Magharibi na nchi kama Saudi Arabia.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani na washirika wake wa Magharibi barani Ulaya na nje ya bara hilo kama Canada, mbali na kutekeza wazi chuki na uadui dhidi ya Iran kama kuliwekea vikwazo vipya taifa hili, daima wamekuwa wakiwachochea na kuwapatia miongozo wafanyafujo hata katika uga wa namna ya kutengeneza mada za milipuko na kusababisha moto wakifanya hima kama wanavyodai kuhakikiisha kwamba, moto wa fitina unaendelea kuwaka nchini Iran. Lengo la hayo yote ni kudhoofisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzusha vurugu, fujo na machafuko ya ndani.
Sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu juu ya kupangwa na kuratibiwa nje ya nchi fujo na ghasia za hivi karibuni hapa Iran ni jambo linalofahamika bayana hasa kwa kutilia maanani uungaji mkono wa pande zote wa uistikbari wa dunia ukiongozwa na Marekani kwa wafanyafujo, kuwaongozwa na kutangaza utayari wa kuchukua hatua za kivitendo za kuwaunga mkono wafanyafujo hao kama vile kuondoa vikwazo vinavyohusiana na intaneti na mitandao ya kijamii.
Pamoja na hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anaamini kuwa, hatua hizo za kutaka kuuangusha mfumo wa Kiislamu ambazo zimekuweko kwa zaidi ya miaka 40 sasa tangu kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hazina ubavu wa kuzuia kasi ya kusonga mbele Jamhuri ya Kiislamu.
Waidha Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Madhali wananchi wa Iran wangali wameshikilia juu bendera ya Uislamu basi daima wapo pamoja na mfumo wa Kislamu na kwa muktadha huo, uadui kwa aina mbalimbali utaendelea kushuhudiwa dhidi ya taifa hili na hapana shaka kuwa, njia pekee ya kukabiliana na maadui na kusimama kidete. Maneno hayo ya Kiongozi Muadhamu ni ishara ya ahadi ya Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu ambapo amewaahidi ushindi waumini endapo watasimama kidete mbele ya maadui.
Jambo jingine ni kuwa, Marekani ambayo inadai na kuonyesha kuwa na uchungu na huruma na wananchi wa Iran na inafanya juhudi za kuondoa vikwazo vinavyohusiana na intaneti na mitandao ya kijamii ili kwa njia hii kama inavyojidanganya iandae uwanja wazi nchini Iran wa kutoa pigo kwa mfumo unaotawala, ndio adui mkubwa kabisa wa taifa hili na imeonyesha wazi hilo mara chungu nzima.
Mfano wa wazi wa uadui wa Marekani kwa Iran ni hatua yake ya kuliwekea taifa hili vikwazo vya kiwango cha juu kabisa katika kipindi cha uongozi wa Donald Trump mwaka 2018, sera ambazo hadi sasa zinatekelezwa kwa nguvu zote na utawala wa Rais wa sasa wa nchi hiyo mwenye maradhi ya kusahau sahau Joe Biden.
Mfano wa hivi karibuni kabisa wa uadui wa Marekani kwa Iran ni vikwazo vipya vya Washington dhidi ya sekta ya usafirishaji wa anga ambavyo kimsingi vinawalenga moja kwa moja wananchi wa Iran na usalama wa safari za anga za taifa hili.
Muhammad Muhammadi-Bakhsh, Mkuu wa Shirika la Anga la Iran anasema kuhusiana na hilo: Licha ya kufanyika mazungumzo na Magharibi, Marekani na Ulaya siyo tu kwamba, hakuna hatua chanya iliyochukuliwa na madola hayo katika sekta ya usafiri wa anga, bali yameweka vikwazo vipya katika sekta ya mafuta na vipuri. Hatua hii inadhihirisha wazi na bayana utambulisho halisi wa mtazamo na utendaji wa Magharibi ikiongozwa na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, utendaji ambao umejengeka juu ya misingi ya uadui mkubwa dhidi ya taifa hili la Kiislamu ambalo limesimama kidete na kukataa kuburuzwa.