Nov 28, 2022 11:40 UTC
  • Nasser Kan'ani: Iran haitatoa ushirikiano wowote kwa 'tume ya kutafuta ukweli'

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa msimamo kuhusiana na azimio dhidi ya Iran la Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, na kueleza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitatoa ushirikiano wowote kwa tume ya kisiasa iliyopewa jina la "tume ya kutafuta ukweli".

Siku ya Alkhamisi,  Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, kwa mwongozo wa Ujerumani, lilipitisha azimio dhidi ya Iran kuhusiana na kile kilichoitwa "hali ya haki za binadamu nchini Iran".
Kupitishwa kwa azimio hilo kunamaanisha kuwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa limeafiki kuundwa "jopo la kutafuta ukweli" juu ya madai ya "kukiukwa haki za binadamu na Iran" katika machafuko ya hivi karibuni.
Nasser Kan'ani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ambaye leo alikuwa na mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi, amegusia hatua ya nchi za Magharibi dhidi ya Iran katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na akasema, kuzitumia kimihemko taratibu za haki za binadamu na kuzitumia pia kiuwenzo na kimaslahi taratibu hizo dhidi ya nchi zenye misimamo huru hakukubaliki na kunalaaniwa, na wala hakutasaidia kivyovyote vile kuboresha haki za binadamu.
Kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la UN

Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameongeza kuwa: hakuna chembe ya shaka kwamba serikali za Magharibi na hasa serikali ya Marekani na baadhi ya zile zinazoifuata Washington zilichangia katika kuchochea machafuko ndani ya Iran, na kuna taarifa za uhakika juu ya hilo; na akabainisha kuwa, taarifa hizo zimewasilishwa kwa mabalozi wa kigeni wanaoishi Tehran kupitia njia tofauti.

Msemaji wa vyombo vya diplomasia vya Iran amesema: kuna idadi kubwa ya raia wa nchi mbalimbali ambao wametiwa mbaroni katika machafuko ya hivi karibuni katika baadhi ya miji ya Iran na kuna ushahidi madhubuti na wa uhakika kuhusu namna walivyochangia kuhamasisha fujo na machafuko.
Kuhusu tuhuma za Marekani dhidi ya Iran kwamba imeshambulia meli ya mafuta ya Israel, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: kuzusha tuhuma hewa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwenendo unaofahamika sana wa Marekani, utawala wa Kizayuni na waitifaki wao; na Jamhuri ya Kiislamu inao ujasiri wa kutosha wa kukiri juu ya mambo yoyote yale inayofanya.
Katika mkutano wake huo na waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi, Kan'ani Chafi ameitakia mafanikio pia timu ya taifa ya kandanda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar na akasema kuhusu kitendo cha timu ya taifa ya Marekani cha kuivunjia heshima bendera ya Iran kwamba: wakati Marekani inajidai kuwa mchungaji maadili na mfuataji sheria, inavunjia heshima bendera ya Jamhuri ya Kiislamu; na akasisitiza kuwa Marekani imefanya uhalifu na kukiuka sheria za FIFA na inapasa iwajibishwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.../

Tags