Mar 27, 2024 12:06 UTC
  • Ulimwengu waunga mkono ripoti ya UN kuhusu mauaji ya kimbari ya Israel Ukanda wa Gaza

Tathmini iliyofanywa na Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Palestina ambayo imezitaja jinai za utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari imeungwa mkono pakubwa na nchi mbalimbali katika umoja huo.

Bi Francesca Albanese Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa Anayehusika na Masuala ya Haki za Binadamu ya Palestina katika Baraza la Haki za Binadamu la UN ameeleza kuwa nchi mbalimbali zinapasa kuuwekea utawala wa Kizayuni vikwazo vya silaha na vinginevyo. 

Shirika la habari la Wanavyuo wa Iran (ISNA) limeripoti kuwa Albanese ambaye jana Jumanne aliwasilisha ripoti yake kuhusu Gaza kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva Uswisi katika ripoti yake hiyo amefikia natija kwamba utawala wa Kizayuni unatekeleza mauaji ya kimbari huko Ukanda wa Gaza. 

Utawala wa Kizayuni unatekeleza mauaji ya kimbari Gaza 

Utawala wa Kizayuni umekadhibisha yale yaliyoelezwa ndani ya ripoti ya Francesca Albanese huku mashinikizo ya kimataifa yakiongozeka kwa utawala huo ili usimamishe vita vyake haraka iwezekanavyo. 

Wakati huo huo makumi ya wanadiplomasia wengi wao wakiwa ni wanadiplomasia wa ngazi za juu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu na pia kutoka Amerika ya Latini wameunga mkono na kupongeza ripoti na hatua zilizochukuliwa na Bi Francesca Albanese Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa Anayehusika na Masuala ya Haki za Binadamu ya Palestina katika Baraza la Haki za Binadamu la UN. 

 

Tags