Apr 27, 2024 11:43 UTC
  • Kongo DR yaituhumu Apple Inc. kwa kutumia

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetishia kuichukulia hatua ya kisheria kampuni ya Apple Inc kwa kushirikiana na watoroshaji wa madini kutoka Kongo DR.

Wanasheria wa serikali ya Kongo wanaituhumu kampuni kubwa ya teknolojia ya Apple Inc. kuwa inanunua madini yaliyotoroshwa kutoka migodini mashariki mwa Kongo ambako waasi wanakiuka haki za binadamu na kisha kuyahamishia madini hayo katika nchi jirani ya Rwanda.

Wanasheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameitumia kampuni hiyo kubwa ya kiteknolojia ya Marekani notisi rasmi wakiitaka isitishe kujishulisha na ununuaji madini yaliyotoroshwa kutoka Kongo  na kuonya kuwa huenda wataichukulia hatua za kisheria ikiwa itapuuza onyo hilo. 

Wanasheria hao wa Kongo wenye makazi yao mjini Paris, Ufaransa wameituhumu Kampuni ya Apple kwa kujihusisha na magendo ya madini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuyaingiza katika nchi jirani ya Rwanda ambako hutakatishwa na kisha kuingizwa katika mnyororo wa soko la kimataifa. 

Madini hayo ni pamoja na bati, tantalum na cobalt ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za teknolojia ya juu yanayochimbwa na makundi yanayobeba silaha katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko mashariki mwa Kongo. 

Apple Inc. yatuhumiwa kutorosha madini ya Kongo 

Maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yenye utajiri mkubwa wa madini yamekumbwa na machafuko na ukosefu wa amani huku waasi wa M23 wakiwania kudhibiti maeneo hayo. 

serikali ya Kinshasa na Umoja wa Mataifa zinaituhumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi wa M23 ili kudhibiti maeneo hayo tajiri kwa madini; tuhuma ambazo zimekanushwa na serikali ya Kigali. 

Tags