Apr 27, 2024 08:07 UTC
  • Marekani kuwaondoa wanajeshi kutoka Chad kufuatia mashinikizo

Kufuatia mashinikizo Marekani inapanga kuondoa baadhi ya wanajeshi wake kutoka Chad siku chache baada ya kutangaza kuondoka kwa vikosi vyake kutoka nchi jirani ya Niger.

Uondoaji wa vikosi maalum vya 75 vya Marekani umeripotiwa kupangwa kuanza wikendi hii na utakamilika ndani ya siku chache. Marekani ina takriban wanajeshi 100 nchini Chad, kwa kisingizio cha kupambana na itikadi kali.

Katibu wa vyombo vya habari wa Pentagon Meja Jenerali Pat Ryder amenukuliwa akisema kwa sasa Marekani inapanga kupanga upya baadhi ya vikosi vyake vya kijeshi kutoka Chad na baadhi tayari vinapangwa kuondoka.

Wiki iliyopita Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga la Chad alisema kuwa hajapokea nyaraka zozote kutoka kwa Wamarekani "zinazoonyesha sababu ya wao kuhitajia kuwepo katika Uwanja wa Ndege za Kijeshi wa Adji Kosseï (BAK)" katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena.

Katika miezi ya hivi karibuni, nchi za ukanda wa Sahel barani Afrika zimeanza kutilia shaka malengo ya uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo.

Mnamo Machi, serikali ya Niger ilitangaza kuwa itasitisha makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Marekani. Niger imesisitiza kuwa uwepo wa jeshi la Marekani nchini humo ni kinyume cha sheria kwa Niger.