Apr 27, 2024 10:43 UTC
  • Iran Expo 2024, maonyesho ya uwezo wa kiuchumi wa Iran

Maonesho ya sita ya uwezo wa kusafirisha nje bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRAN EXPO 2024) yameanza leo mjini Tehran kwa lengo la kuonesha uwezo wa kiuchumi wa Iran.

Maonyesho ya 6 ya IRAN EXPO 2024, ambayo mamefunguliwa rasmi na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni tukio kubwa zaidi la mauzo ya nje ya bidhaa za Iran, na yanawashirikisha wafanyabiashara zaidi ya elfu mbili wa kigeni kutoka nchi 119. Maonyesho hayo yataendelea hadi tarehe Mosi Mei.

Miongoni mwa malengo ya Iran Expo 2024 ni kutayarisha jukwaa linalofaa kwa ajili ya uwekezaji wa sekta ya viwanda ya Irani katika nchi mbalimbali na kuvutia wawekezaji wa kigeni. Iran Expro 2024 ni maonyesho ya kitaifa ambayo yanaonyesha uwezo halisi wa nchi katika uwanja wa mauzo ya nje.

Maonyesho ya Iran Expo 2024 yana sifa mbili muhimu. Ya kwanza ni ushiriki mkubwa wa wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali ili kujua uwezo wa kiuchumi wa Iran na vilevile uwezo wa makampuni ya kibiashara ya nchi hiyo. Sifa nyingine muhimu ya maonyesho haya ni utayarifu wa makampuni ya Iran kwa ajili ya uwekezaji na shughuli za kiuchumi katika maeneo yote ya dunia ili sekta ya viwanda iweze kutambulisha bidhaa na uwezo wake wa kiufundi kwa nchi nyingine.

Sehemu ya maonyesho ya Iran Expo

Maonesho ya 6 ya Iran Expo yanafanyika katika hali ambayo makampuni ya Iran yameweza kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kiufundi wa kuzalisha bidhaa mbalimbali licha ya vikwazo vilivyowekwa na Marekani na washirika wa Magharibi wa Ikulu ya White House; na licha ya vikwazo vyote hivyo, makampuni hayo yamekuwa na nafasi muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa kisayansi wa Iran.

Katika miaka ya hivi karibuni wanasayansi na wataalamu vijana wa Iran wamefanikiwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na wamekidhi mahitaji ya nchi katika nyanja mbalimbali kwa kiasi kikubwa. Maonesho ya Iran Expo pia yana nafasi maalumu katika kuarifisha bidhaa za Iran.

Abbas Aliabadi, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran amesema kuhusu uwepo wa wafanyabiashara wa kigeni katika maonesho ya mwaka huu ya IRAN EXPO kwamba: Wafanyabiashara hao elfu mbili wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa Iran, na iwapo kutasainiwa mikataba ya kibiashara, suala hilo litakuwa na taathira kubwa na kuwa chachu katika kazi na ajira na hali bora ya jamii.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, maonyesho haya ni njia ya kutambulisha uwezo wa kiuchumi wa Iran na nafasi yake katika ngazi ya dunia. Iran, ambayo ina rasilimali tajiri na miundombinu inayofaa ya kiuchumi, pamoja na nguvu kazi ya wataalamu na vijana, ina sehemu kubwa katika soko la kiuchumi la kimataifa, na Expo 2024 ni fursa ya kutambulisha bidhaa za makampuni ya Iran.