Rais Rouhani: Iran itaendelea kuzisaidia nchi jirani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i9262-rais_rouhani_iran_itaendelea_kuzisaidia_nchi_jirani
Rais Hassan Rouhani amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuzisaidia nchi jirani kwa madhumuni ya kurejesha amani na usalama katika nchi hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2016 11:06 UTC
  • Rais Rouhani: Iran itaendelea kuzisaidia nchi jirani

Rais Hassan Rouhani amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuzisaidia nchi jirani kwa madhumuni ya kurejesha amani na usalama katika nchi hizo.

Akizungumza baada ya kikao cha wakuu wa mihimili mitatu ya dola ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambacho pamoja na mambo mengine kimechunguza matukio yanayojiri katika Mashariki ya Kati, Rais Rouhani amesema hali ya mambo katika eneo hivi sasa si ya kuridhisha kwa sababu mauaji yanaendelea na magaidi nao wanaendeleza vitendo vyao ya kinyama huku itibari ya taasisi za kimataifa ikiendelea kupungua kila siku.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kulegeza msimamo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mbele ya mashinikizo ya nchi moja tu kwa sababu ya kutishia kutotoa fedha ili jina la nchi hiyo liondolewe kwenye orodha ya wakiukaji haki za watoto kunaonyesha kuwa jumuiya za kimataifa hazina tena hata ile hadhi yenye kasoro ambayo zilikuwa nayo huko nyuma.

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa njia pekee ya utatuzi wa migogoro katika nchi za eneo ni kwa wananchi wenyewe wa mataifa hayo kutumia vizuri kujitawala kwao ili kurejesha amani na uthabiti katika nchi zao na kuongeza kuwa anatumai kwamba amani na uthabiti itarejea haraka katika nchi za Iraq na Syria, na magaidi watatimuliwa katika ardhi za nchi hizo.../