Rais Ebrahim Raisi: Taifa la Iran muda wote limekuwa likiwakatisha tamaa maadui
(last modified Fri, 03 Feb 2023 04:14:00 GMT )
Feb 03, 2023 04:14 UTC
  • Rais Ebrahim Raisi: Taifa la Iran muda wote limekuwa likiwakatisha tamaa maadui

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kujitokeza vilivyo na kwa wingi wananchi katika nyuga tofauti kumekuwa muda wote kukiwavunja moyo na kuwakatisha maadui wa Iran ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana (Alkhamisi) wakati alipoonana na wajumbe wa "Kamati Kuu ya Maadhimisho ya Alfajiri Kumi."

Aidha sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Jawad AS na Imam Ali AS na kuwadia maadhimisho ya mwaka wa 44 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, wananchi wenye muono wa mbali na waliopevuka kifikra wa Iran ya Kiislamu huwa wanatumia matukio tofauti kama yale ya Aban 13, kutangaza imani yao kwa Jamhuri ya Kiislamu na kumkatisha tamaa adui.

Kila mwaka matukio kama hayo huwa yanafana zaidi kuliko mwaka wa kabla yake na hii inaonesha wazi kuwa, wananchi Waislamu wa Iran wamesimama imara kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo waliojichagulia kwa ridhaa yao, yaani wa Jamhuri ya Kiislamu. 

Maadhimisho ya Bahman 22. Hali yoyote ya hewa haiwazuii wananchi wa Iran kujitokeza kwa mamilioni katika maadhimisho hayo.

 

Rais wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran vile vile amesema, katika matukio ya hivi karibuni, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alitoa ufafanuzi wa kina na muhimu sana kuhusu sababu za fitna hiyo ya adui na kwamba miongozo yake hiyo imesaidia sana katika kupambana na kufelisha njama hizo za adui.

Rais Raisi aidha amesema, adui anafanya njama za kila namna kujaribu kulikwamisha taifa la Iran lisifikie malengo yake matukufu, lakini amesema, serikali yake ambayo ni ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kufanya mazungumzo ya kuondolewa vikwazo kwa kulinda kikamilifu heshima ya taifa hili na haitoruhusu kukwama harakati yoyote ya maendeleo humu nchini.

Tags