Feb 16, 2023 07:54 UTC
  • Alena Douhan
    Alena Douhan

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa, vikwazo vya Washington dhidi ya taifa la Iran na hatua zake dhidi ya nchi nyingine ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Alena Douhan na Obiora C. Okafor, maripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wameeleza athari mbaya za vikwazo vya upande mmoja na haramu vya Marekani kwa Wairani wanaougua thalassemia (ugonjwa wa upungufu wa damu mwilini) na kutangaza kuwa, dawa za wagonjwa wa thalassemia zimetengezwa na kampuni ya Uswisi ya Novartis na viungo vyake pia vilitoka kwa kampuni ya Ufaransa, lakini kutokana na vikwazo vya Marekani, dawa hizi hazifiki Iran.

Douhan na Okafor wanasema kwamba hata ruhusa inapotolewa, watengenezaji, wasafirishaji, bima au benki wanasitasita kufanya biashara na Iran kutokana na hofu ya vikwazo vya uhasama ya Marekani, na suala hili linasababisha hofu, maumivu na vifo vya mapema vya wagonjwa wa thalassemia.

Maripota hawa wawili maalumu wa Umoja wa Mataifa wameiomba serikali ya Marekani kuondoa vikwazo na vizuizi vyovyote katika miamala ya kifedha kwa madhumuni ya kutoa huduma za matibabu, na kutoweka vikwazo vya ziada kwa makampuni yanayouza dawa kwa Iran.

Pir-Hossein Kolivand, Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Irani alisema hivi karibuni katika mkutano wa mashauriano wa wakuu wa jumuiya za kitaifa za Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu za Asia Magharibi na Afrika Kaskazini (MENA) huko Beirut kwamba: Vikwazo vya kikatili vimeathiri shughuli za kibinadamu za jumuiya ya Hilali Nyekundu na kuizuia kutekeleza ipasavyo wajibu na majukumu yake katika ngazi za ndani na kimataifa.

Vikwazo vya serikali ya Marekani vimekuwa na taathira mbaya zaidi katika sekta ya dawa na tiba ya Iran katika miaka ya hivi karibuni.

Tags