Amir-Abdollahian: Mlango wa mazungumzo bado uko wazi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94332-amir_abdollahian_mlango_wa_mazungumzo_bado_uko_wazi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema jana Jumanne mbele ya Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kwamba, mlango wa mazungumzo bado uko wazi na bado Tehran inaendelea kubadilishana ujumbe mbalimbali na pande husika za mazungumzo hayo kupitia wapatanishi.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Feb 22, 2023 03:00 UTC
  • Amir-Abdollahian: Mlango wa mazungumzo bado uko wazi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema jana Jumanne mbele ya Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kwamba, mlango wa mazungumzo bado uko wazi na bado Tehran inaendelea kubadilishana ujumbe mbalimbali na pande husika za mazungumzo hayo kupitia wapatanishi.

Msemaji wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran, Abolfazl Amoui ametoa ufafanuzi kuhusu kikao cha jana Jumanne cha kamisheni hiyo kilichohudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na kusema: Waziri wa Mambo ya Nje aliwasilisha ripoti ya ziara ya rais na mawaziri alioandamana nao mjini Beijing na kusema kwamba, China inauhesabu uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni wa kimkakati na wa kiistratijia na ndio maana inaupa umuhimu mkubwa ushirikiano huo. Kulingana na mazungumzo yaliyofanyika baina ya pande hizo, kumetiwa saini hati 19 zinazogusa maeneo mbali mbali kama utengenezaji wa magari, teknolojia, mazingira na ushirikiano katika nishati ya nyuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa mlango wa mazungumzo bado uko wazi

 

Amoui amesema: Hati hizo zinaendeleza dira ya ushirikiano wa miaka 25 kati ya Iran na China, ambao ulitiwa saini na pande hizi mwaka jana wa 2022. Maelezo ya baadhi ya hati hizi yatakuwa mikataba ambayo itawekwa wazi kwa ajili ya kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Iran na China.

Msemaji wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Bunge la Iran pia amesema: Kwa kuzingatia maelezo yaliyotolewa, ujumbe wa Iran mjini Beijing umepokewa kwa heshima kubwa na kwa hadhi ya hali ya juu, jambo ambalo linaonyesha juhudi za serikali ya China katika kuendeleza na kuimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.