Iran yapanga vikwazo vya kulipiza kisasi dhidi EU, Uingereza
Iran imetangaza kuweka vikwazo vya kulipiza kisasi dhidi ya idadi kadhaa ya watu binafsi na mashirika katika Umoja wa Ulaya (EU) na Uingereza.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitangaza hatua hizo katika taarifa yake siku ya Jumanne. Jumatatu iliyopita wizara hiyo ilikuwa imeonya kwamba italipiza kisasi dhidi ya hatua kama hizo zilizochukuliwa hapo awali na Baraza la Umoja wa Ulaya na Uingereza dhidi ya idadi kubwa ya Wairani na taasisi za Kiirani kutokana na hatua ilizochukua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukabiliana na ghasia zinazoungwa mkono na mataifa ya kigeni zilizozuka katika baadhi ya miji ya Iran mnamo Septemba mwaka jana.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitaja baadhi ya sababu za kupitishwa kwa hatua hizo za kuwa ni "uungaji mkono wa EU na Uingereza kwa ugaidi na vikundi vya kigaidi" na "uchochezi wao wa vitendo vya ugaidi na unyanyasaji dhidi ya watu wa Iran."
Mashirika ya usalama ya Iran yamepata ushahidi kuwa mashirika ya ujasusi ya Marekani na madola mengine ya Magharibi yalihusika katika ghasia hizo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imeulaumu umoja huo na Uingereza kwa "kuingilia mambo ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu," na "kueneza uwongo na habari potofu kuhusu Iran."
Halikadhalika Iran imekosoa ushirikiano wa nchi za Ulaya na vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hiyo, ambavyo vimefikia kiwango cha "ugaidi wa kiuchumi."
Taarifa hiyo imetaja hatua za EU na Uingereza za kuwezesha vitendo vya ugaidi na uharibifu dhidi ya taifa la Iran kuwa ni "ukiukaji wa majukumu yao ya kimataifa katika uwanja wa kupambana na ugaidi."