Amir-Abdollahian: Iran daima inakaribisha diplomasia, haijawahi kujitenga na mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94506-amir_abdollahian_iran_daima_inakaribisha_diplomasia_haijawahi_kujitenga_na_mazungumzo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema Iran daima imekuwa ikiunga mkono njia ya kidiplomasia ya utatuzi wa hitilafu na haijawahi kujiweka mbali na meza ya mazungumzo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2023 04:24 UTC
  • Amir-Abdollahian: Iran daima inakaribisha diplomasia, haijawahi kujitenga na mazungumzo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema Iran daima imekuwa ikiunga mkono njia ya kidiplomasia ya utatuzi wa hitilafu na haijawahi kujiweka mbali na meza ya mazungumzo.

Ameyasema hayo katika mahojiano maalum na Kanali ya Televisheni ya Al-Alam ya Iran, ambapo amezungumzia ziara yake ya hivi majuzi mjini Baghdad na mikutano yake na viongozi wa ngazi za juu wa Iraq akiwemo waziri mwenzake, Fuad Hussein. Amir-Abdollahian amedokeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amerejea kutoka katika ziara yake ya hivi karibuni mjini Washington akiwa na ujumbe kwa Iran.

Akifafanua amesema, "alibeba ujumbe kwamba upande wa Marekani uko tayari kwa makubaliano na Iran juu ya kufufua mapatano ya nyuklia ya 2015, yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA)."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, daima Iran inakaribisha njia ya diplomasia na mazungumzo na wala haijawahi kujiweka mbali na mazungumzo.

Ameongeza kuwa Iran iko tayari kuchukua hatua kufikia mapatano ya JCPOA na kuhakikisha wote waliotia saini mapatano hayo wanatekeleza ahadi zao ndani ya fremu ya mazungumzo yaliyofanyika katika mji mkuu wa Austria, Vienna.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesisitiza kuwa, makubaliano yoyote ya aina hiyo ni lazima yadhamini maslahi ya pande zote, huku yakiheshimu pia mistari miekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amir-Abdollahian amesema ikiwa upande wa Marekani utachukua hatua kihalisia ndani ya mfumo wa ujumbe wake na kuepuka kurudia matamshi yake ya kinafiki katika vyombo vya habari, hatutakuwa mbali na makubaliano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza, "Tatizo, hata hivyo, ni kwamba Wamarekani daima hutoa taarifa za kidiplomasia zinazokinzana na wanayotamka katika vyombo vya habari. Tunatumai kwamba wakati huu Wamarekani watachukua hatua kwa kuzingatia uhalisia wa mambo na waepuke kuwa wanafiki.”

Iran imethibitisha kuwa  mpango wake wa nyuklia ni wa malengo ya amani kwa ulimwengu kwa kutia saini makubaliano ya JCPOA na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani. Hata hivyo, hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujitoa katika mapatano hayo Mei 2018 na baadaye kuweka tena vikwazo dhidi ya Iran ndio chanzo cha kuvurugika mapatano hayo. Mazungumzo ya kuhuisha mapatano hayo ambayo yamekuwa yakifanyika Vienna, Austria  hayajafanikiwa kutokana na ukaidi wa Marekani.