Eslami: Faili la masuala yanayozozaniwa baina ya Iran na IAEA limeshafungwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94590-eslami_faili_la_masuala_yanayozozaniwa_baina_ya_iran_na_iaea_limeshafungwa
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesisitiza kuwa, faili la masuala yanayozozaniwa baina ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), limeshafungwa tayari.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2023 07:36 UTC
  • Eslami: Faili la masuala yanayozozaniwa baina ya Iran na IAEA limeshafungwa

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesisitiza kuwa, faili la masuala yanayozozaniwa baina ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), limeshafungwa tayari.

Mohammed Eslami amesema hayo leo Jumatano pembeni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri kilichojadili namna Iran inavyoshirikiana na wakala wa IAEA na kusema, masuala yaliyokuwa yanazozaniwa baina ya pande hizo mbili yameshatatuliwa. 

Aidha amesema, mawasiliano yanaendelea baina ya Iran na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na manaibu wake na hivi sasa wajumbe wa IAEA wapo hapa mjini Tehran kwa ajili ya kufuatilia masuala ya kiufundi ya mradi wa nyuklia wa Iran.

Mwishoni mwa mwezi ulioisha wa Februari pia yaani siku ya Jumapili, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) alisema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inajiandaa kuanza kusafirisha nje ya nchi bidhaa zake za nyuklia, zikiwemo za tiba.

Shirika la habari la IRNA lilimnukuu Mohammed Eslami akisema hayo siku hiyo ya Jumapili katika awamu ya 29 ya Mkutano wa Nyuklia uliofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Shahid Beheshti mjini Tehran na kuongeza kuwa, wanasayansi wa nyuklia wa Iran wamepata mafanikio makubwa katika mwaka unaomalizika wa Kiirani wa 1401 Hijria Shamsia. Mwaka huo wa Kiirani wa Hijria Shambua, utaisha tarehe 20 mwezi huu wa Machi.

Muhandisi Eslami vile vile alisema, Iran imefanikiwa kuzalisha poda maalumu inayotumika kudhibiti kuvuja na kuganda damu wakati wa upasuaji, bidhaa muhimu ambayo Iran ilishindwa kuiagiza kutoka nje ya nchi kutokana na vikwazo vya maajinabi. Alisema, hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu itaanza kuiuza bidhaa hiyo muhimu nje ya nchi.