Iran yawatimua wanadiplomasia wawili wa Ujerumani kwa kuingilia masuala ya ndani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa amri ya kufukuzwa wanadiplomasia wawili wa Ujerumani kutokana na kuingilia masuala ya ndani ya nchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Ujerumani kukosoa uamuzi wa Jamhuri ya Kiislamu wa kutoa hukumu ya kifo kwa kiongozi wa kundi la kigaidi lenye makao yake makuu nchini Marekani, ambalo limetekeleza mashambulizi kadhaa ya kigaidi nchini.
Nasser Kana'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, alitangaza Jumatano kwamba wanadiplomasia hao wawili wa Ujerumani wametangazwa kuwa "watu wasiotakikana" na kuamriwa kuondoka nchini mara moja kutokana na "hatua za kutowajibika na uingiliaji wa serikali ya Berlin katika masuala ya ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na kuingilia masuala ya mahakama ya Iran.
Kana'ani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua hatua madhubuti dhidi ya wanaoingilia masuala ya ndani ya nchi huku akiashiria kuitwa kwa balozi wa Ujerumani mjini Tehran katika Wizara ya Mambo ya Nje ili kujulishwa kuhusu uamuzi huo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ilitangaza katika taarifa Jumatano kwamba wafanyakazi wawili wa Ubalozi wa Iran huko Berlin wamefukuzwa nchini humo.
Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Mahakama ya Iran kumhukumu kifo raia wa Iran Jamshid Sharmahd ambaye pia ana uraia wa Ujerumani kwa kosa la kueneza ufisadi katika ardhi kwa kupanga na kuratibu vitendo vya kigaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alitoa kauli isiyofaa baada ya kutolewa hukumu hiyo huku akiishutumu Jamhuri ya Kiislamu kwa kile alichodai ni "ukiukaji mkubwa wa haki za raia wa Ujerumani."
Sharmahd, ambaye pia ni mkazi wa Marekani, alikuwa kinara wa kundi la kigaidi la Tondar. Alishtakiwa kwa kupanga mfululizo wa mashambulizi, ikiwa ni pamoja na shambulio la mwaka 2008 dhidi ya kituo cha kidini katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran, Mkoa wa Fars, ambalo liliua watu 14 na kujeruhi mamia ya wengine.