Kamalvandi: Iran na IAEA zimeafikiana kushirikiana zaidi
Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran amesema mapatano ya hivi karibuni kati ya Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki yaliyofikiwa wakati wa safari ya mkurugenzi mkuu wa wakala huo yanaenda sambamba na sheria ya kimkakati iliyopitishwa na Bunge la Iran.
Behrouz Kamalvandi ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika Rasmi la Habari la Iran, IRNA, ambayo yamechapishwa mapema leo Jumapili.
Jana Iran na IAEA zilitoa taarifa na kusema zimeafikiana kuchukua hatua za kushirikiana na kuharakisha utatuzi wa masuala yaliyosalia baina ya pande mbili.
Taarifa hiyo imetokelewa baada ya safari ya siku mbili nchini Iran ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atoiki (IAEA) Rafael Grossi ambapo alikutana na Rais wa Iran Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran Mohammad Eslami.
Pande mbili ziliafikia kuwa maingiliano ya pande mbili yanapaswa kutekelezwa kwa moyo wa ushirikiano huku Iran ikitangaza kuwa tayari kuendeleza ushirikiano wake na kutao taarifa zinazohitajika na wakala huo kuhusu masuala yaliyosalia ya usalama wa kinyuklia.
Kamalvandi amesema mapatano hayo ya Iran na IAEA yanaenda sambamba na sheria iliyopitishwa na Bunge la Iran mnamo Disemba 2020 kuhusu kuimarisha mchakato wa ustawi wa mango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.
Jana Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raeisi, Katika kikao na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi, alisema Tehran inatarajia IAEA itachukua mtazamo wa "kitaalamu" kuhusu mpango wa Iran wa nishati ya nyuklia na kujiepusha kuathiriwa na baadhi ya madola ambayo yanafuatilia malengo ya kisiasa.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran Mohammad Eslami mapema siku ya Jumamosi, Grossi alisema shambulio lolote la kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia ni marufuku. Kauli hiyo ilikuwa ya kujibu vitisho vya Marekani na Israel vya kutaka kulenga vituo vya nyuklia vya Iran.
Akiwa mjini Tehran Grossi pia amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ambapo amesema ni "suala la lazima kuwa na mazungumzo ya kina na Iran."