Kana'ani: Marekani iliunga mkono mfumo wa 'apartheid' Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94760
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani haistahiki kujipiga kifua na kudai kuwa kinara wa kutetea na kulinda haki za binadamu duniani kutokana na rekodi yake nyeusi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 05, 2023 11:10 UTC
  • Kana'ani: Marekani iliunga mkono mfumo wa 'apartheid' Afrika Kusini

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani haistahiki kujipiga kifua na kudai kuwa kinara wa kutetea na kulinda haki za binadamu duniani kutokana na rekodi yake nyeusi.

Nasser Kana'ani amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamiii wa Twitter leo Jumapili na kueleza kuwa, Marekani iliunga mkono mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid nchini Afrika Kusini, na kwa msingi huo haina haki ya kujinadi kuwa mtetezi wa haki na demokrasia.

Kana'ani ameeleza bayana kuwa, "Kuna wakati Marekani iliunga mkono utawala wa apartheid nchini Afrika Kusini, na (Shirika la Ujasusi la Marekani) CIA lilihusika katika kukamatwa (Nelson) Mandela, aliyekuwa kiongozi wa mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Hii leo, Marekani ni muitifaki wa kistratajia na mtetezi wa utawala wa kibaguzi na Kizayuni wa Israel, haipasi kujifanya inalinda haki za binadamu na demokrasia. Haina imani kamwe na masuala hayo (haki za binadamu na demokrasia).

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, Richard Stengel, ripota wa zamani wa jarida la Time, aliandika katika makala yake kwamba: Ripoti mpya ya uchunguzi inaonyesha kwamba Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) huenda lilihusika katika kukamatwa kwa Nelson Mandela, kiongozi wa upinzani dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Baada ya kuongoza harakati ya kupinga ubaguzi wa rangi, Mandela alikuwa mzalendo mweusi wa kwanza kushika wadhifa wa urais wa Afrika Kusini kuanzia mwaka 1994 hadi 1999.