Amir-Abdollahian : Iran katu haitaacha kuunga mkono Palestina, muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94836-amir_abdollahian_iran_katu_haitaacha_kuunga_mkono_palestina_muqawama
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitarudi nyuma hata chembe moja kuhusu msimamo wake wa kuunga mkono muqawama na kupigania ukombozi wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 07, 2023 08:43 UTC
  • Amir-Abdollahian : Iran katu haitaacha kuunga mkono Palestina, muqawama

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitarudi nyuma hata chembe moja kuhusu msimamo wake wa kuunga mkono muqawama na kupigania ukombozi wa Palestina.

Akihutubia 'Kongamano la Diplomasia ya Muqawama' mjini Tehran siku ya Jumanne, Amir-Abdollahian amesema Wairani wote wataendelea kushikamana na kadhia ya Palestina hadi kuanzishwa serikali ya umoja Palestina  ambayo mji mkuu wake ni al-Quds (Jerusalem).

Kwingineko katika matamshi yake, Amir-Abdollahian ameashiria kusimama kidete Iran katika "njia ya diplomasia na mazungumzo" ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya 2015 na kueleza azma ya Tehran ya kuendelea na jitihada zake za kufikia makubaliano kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa.

Ameongeza kuwa Iran kamwe haitajiondoa katika meza ya mazungumzo na imethibitisha kwamba haijawahi kulegeza msimamo kuhusu mstari wake mwekundu hata wakati wa ghasia za hivi majuzi nchini zilizoungwa mkono na madola hasimu ya kigeni.

Iran imeionyesha dunia kuwa mpango wake wa nyuklia unafuatilia malengo ya amani kwa kutia saini makubaliano ya nyuklia, ambayo yanajulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA) na mataifa sita ya dunia - yaani Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Russia na China. Kujiondoa Washington kwa upande mmoja katika mapatano hayo mwezi Mei 2018 na baadae kuweka tena vikwazo dhidi ya Tehran kuliacha mustakabali wa makubaliano hayo ukiwa na utata.

Mazungumzo kati ya pande zinazohusika na mapatano hayo ya nyuklia yalianza mjini Vienna mwezi Aprili 2021, kwa nia ya kuirejesha Marekani katika makubaliano hayo na kusitisha kampeni yake ya "mashinikizo ya juu" dhidi ya Iran.

Majadiliano hayo, hata hivyo, yamesimama tangu Agosti 2022 kutokana na sisitizo la Washington la kutoondoa vikwazo vyote dhidi ya Iran. Aidha Marekani haitaki kutoa hakikisho muhimu kwamba haitajiondoa tena katika makubaliano hayo.