Maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Mahdi AS yafanyika kote nchini Iran
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeungana na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu hii leo kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (AF).
Maeneo tofauti ya Iran ya Kiislamu hususan katika miji mitakatifu ya Mash'had na Qum tangu jioni ya jana ilighariki katika sherehe za maadhimisho ya siku ya kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu, Imam Zama, Mahdi (as).
Kwa mujibu wa Hadithi mbalimbali, leo Jumatano mwezi 15 Shaaban 1444 Hijria inasadifiana na siku ya kuzaliwa Imam Mahdi AS aliyeahidiwa na Bwana Mtume Muhammad (saw) kudhihiri katika zama za mwisho za dunia na kuujaza ulimwengu haki na uadilifu.
Hapa nchini Iran, wapenzi wa Bwana Mtume Muhammad (saw), Ahlul Bayt AS na Imam Mahdi AS wanaadhimisha siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huku msikiti wa Jamkaran katika mjini Qum, (kusini mwa Tehran) ukiwa umefurika mamilioni ya Waislamu kutoka kona mbalimbali za dunia wakiwa na shauku kubwa ya kuona mwokozi huyo wa dunia akidhihiri haraka.

Kwa kawaida, katika siku ya maadhimisho ya kuzaliwa Imam Mahdi AS, Waislamu wa Iran hukusanyika kwenye maeneo matakatifu, misikitini, kumbi za masuala ya kijamii na hata mitaani kufanya sherehe mbalimbali na hasa kuomba dua na kusoma kasida zza kumsifu Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu.
Kwa mujibu wa wanahistoria, Imam Mahdi 9as), mwana wa Imam Hasan al Askari (as) alizaliwa mjini Samarrah Iraq mwezi 15 Shaaban mwaka 255 Hijria. Baba wa mtukufu huyo yaani Imam Hasan al Askari (as), ni Imam wa 11 wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Kuzaliwa mtukufu huyo kulitimia kwa siri, na watu wengi hawakuweza kujua kuzaliwa kwake isipokuwa wafuasi waaminifu wa Imam Hasan al Askari (as) kutokana na ukandamizaji mkubwa wa watawala wa wakati huo, ambao waliweka ulinzi mkali nyumbani kwa mtukufu huyo ili kujaribu kuzuia kuzaliwa Imam Mahdi (as). Hata hivyo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alizaliwa. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.